Friday, September 11, 2015

WAJASIRIAMALI NAMTUMBO WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

WAJASIRIAMALI wadogo wilaya ya Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wamehimizwa kuchangamkia fursa katika maeneo maalumu yaliyotengwa wilayani humo, kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya biashara na shughuli nyingine za ujasiriamali ili waweze kuepukana na usumbufu wanaoupata, kwa kufanya shughuli zao kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwia.

Halmashauri ya wilaya hiyo, imetenga viwanja zaidi ya 300 ambavyo hivi karibuni baada ya taratibu husika kukamilika vitaanza kugawiwa kwa watu wa makundi yote, kwa ajili ya ujenzi wa vibanda hivyo.

Kwa ujumla ugawaji huo utafanywa karibu na eneo linalotarajiwa kujengwa kituo kipya cha mabasi Namtumbo mjini, huku ikisisitizwa kuwa zoezi hilo litapewa kipaumbele zaidi kwa watu waliojiunga kwenye vikundi ambavyo, hujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.


Afisa maendeleo wa wilaya hiyo, Martin Mtani alisema hayo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya kuongeza ubora wa zao la muhogo kwa vikundi vitano vya wajasiriamali wadogo, wilayani humo.

Mafunzo hayo, yaliendeshwa na Muungano wa Vikundi vya Ujasiriamali Vijijini (MUVI) chini ya ufadhili wa shirika la kimataifa, la maendeleo ya kilimo (IFAD) ambayo yalifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo uliopo mjini hapa.

Alisema kuwa ujenzi wa vibanda hivyo, utasaidia kupunguza kero wanazopata wajasiriamali hao kuondolewa katika maeneo ambayo sio rasmi, wanayofanyia biashara bila kufuata taratibu na mipango ya halmashauri husika.

Vikundi vilivyoshiriki ni; Amani, Mshikamano, Juhudi, Tuondoke na Chengena ambavyo licha ya kuzalisha bidhaa bora za muhogo pia vikundi hivyo vinakabiliwa na changamoto ya maeneo ya kufanyia biashara, licha ya kuzalisha bidhaa zao ambapo mwisho wa siku hujikuta wakishindwa kutimiza malengo yao.

Mtani alisema hivi sasa wajasiriamali wengi wamekuwa na tabia ya kumwaga bidhaa zao chini, katika maeneo ya barabarani ambayo sio rasmi kufanyia shughuli hizo.

“Tumeanza mchakato wa ujenzi wa vibanda vya biashara katika eneo litakalokuwa kituo kipya cha mabasi, ni wakati sasa ndugu zangu wa kuchangamkia fursa hii kupata maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vitakavyowasaidia kutangaza na kufanya shughuli zenu”, alisema Mtani.

Katika hatua nyingine, alisema kuwa halmashauri katika msimu wa mwaka 2015/2016 imetenga vituo vya kuuzia na kununua mazao ya chakula na biashara (Buy Centers) ambavyo vitamwezesha mkulima na mfanyabiashara, kuuza na kununua mazao hayo kwa urahisi zaidi.

Vilevile shilingi milioni 10 zimetengwa wilayani humo, ambazo zitatumika kuwajengea uwezo vikundi vinavyojishughulisha na shughuli za kiuchumi ambavyo kupitia mpango wa maendeleo wa wilaya hiyo, kila kikundi kitapewa gawio husika kutoka katika fedha hizo kwa ajili kufanikisha malengo waliyojiwekea.


Pamoja na mambo mengine Ofisa maendeleo ya jamii, Mtani amewataka kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika, ili kuweza kuwavutia wateja wengi kwenda kununua bidhaa hizo.

No comments: