Friday, September 4, 2015

BABA ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUFANYA MAPENZI NA MWANAE

Na Steven Augustino,
Songea.

MKAZI mmoja anayeishi katika mtaa wa Lizaboni Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Abdalah Bakari (43) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma ya kumwingilia kimapenzi mtoto wake wa kike, mwenye umri wa miaka 11.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 10 mwaka huu majira ya usiku, baada ya binti huyo (Jina tunalo) kwenda kulalamika kwa majirani zake, juu ya unyama huo aliofanyiwa.

Akifafanua juu ya tukio hilo, Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa binti huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Amani iliyopo mjini hapa, alidai kuanza kufanyiwa kitendo hicho na baba yake huyo mzazi mwanzoni mwa mwezi wa saba mwaka huu.

Msikhela alisema baba huyo ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Tunduru mkoani humo, imebainika kuwa alikuwa na mazoea ya kumfanyia mtoto huyo unyama huo mara kwa mara jambo ambalo mtoto, alishindwa kuendelea kuvumilia juu ya maumivu aliyokuwa akiyapata na kulazimika kwenda kutoboa siri hiyo, kwa majirani aliokuwa akiishi nao hapo mtaani.


Baada ya siri hiyo kufichuka, ndipo majirani hao walimshauri binti huyo amtafute mtu aliyekuwa jirani na mama yake amweleze maswaibu hayo yaliyomkuta, kisha waende Polisi kutoa taarifa.

Alisema kuwa baada ya mtoto huyo kufanya hivyo na Polisi kupewa taarifa kamili juu ya tukio hilo, walikwenda kumkamata mtuhumiwa na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika atafikishwa Mahakamani, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.


Hata hivyo Kamanda Msikhela, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma ambao wanataarifa juu ya watoto wanaofanyiwa unyama kama huo, watoe taarifa kwa kiongozi wa dawati la jinsia na watoto mkoani humo, kwa kumpigia simu namba ; 0755 761193 au namba ya Kamanda wa Polisi wa mkoa; 0715 009956.

No comments: