Friday, September 4, 2015

DED NAMTUMBO AWAONYA WATUMISHI WAKE KUTOJIINGIZA KWENYE SIASA

Na Mwandishi wetu,
Ruvuma.

SERIKALI wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, imewaonya watumishi wake na kuwataka kutojiingiza katika vitendo vya kushabikia na kuzungumzia mambo siasa wakiwa ofisini, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na maadili mahali pa kazi.

Imeelezwa kuwa kufanya hivyo kunapunguza muda wa kuwatumikia wananchi, badala yake waongeze juhudi kutekeleza majukumu yao waliyopewa na serikali ili kuweza kuleta tija katika jamii, ikiwemo upatikanaji wa huduma muhimu kwa faida ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya hiyo, Ally Mpenye alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya taratibu za maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika, oktoba 25 mwaka huu kwa nafasi ya Rais, diwani na mbunge ambapo kwa mamlaka aliyonayo yeye ndiye msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ndani ya wilaya.


Mbali na hilo, Mpenye pia amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watumishi wa serikali kutumia ofisi za umma kuzungumzia mambo ya kisiasa huku wakisahau jukumu lao la kuwatumikia wananchi bila kujali itikadi ya vyama, dini au kabila ambao hufika katika ofisi zao wakihitaji kupatiwa huduma kwa njia ya ushauri, utaalamu na mawazo mbalimbali ili waweze kutatua na kuondoa kero zao kwa namna moja au nyingine.

“Mimi ndiye kiranja mkuu ndani ya halmashauri, nimekwisha keti na watumishi wenzangu wanaonihusu kwa idara zote hapa wilayani na kuwaeleza wasitumie ofisi za walipa kodi kuzungumzia siasa, siwakatazi kuwa na itikadi za vyama isipokuwa wanatakiwa kufanya hivyo pale wanapotoka nje ya ofisi zao”, alisema Mpenye.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, alisema kuwa licha kupiga marufuku mtumishi kushabikia siasa katika eneo la kazi, kadhalika hakuna ruhusa kwa mtumishi yeyote kuingia ndani ya jengo la halmashauri akiwa amevaa sare ya chama chochote cha siasa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo alisema kuwa ofisi yoyote ya serikali ni ya kila mwananchi, ukizingatia kwamba wao ndiyo walipa kodi wanaoiwezesha ofisi hiyo iweze kufanya kazi hivyo ni kosa kwa mtumishi aliyepewa dhamana na serikali kumtumikia mwananchi, kuvaa sare ya chama fulani wakati anapokuwa ofisini kwa atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.


Alisema kwa mtumishi wa umma, hakatazwi kuwa na mapenzi kwa chama cha siasa anachokitaka isipokuwa mapenzi yake anatakiwa akayaonyeshe mara baada ya kutoka nje ya ofisi hizo, ili kuepuka mifarakano inayoweza kutokea kati yao na wananchi pale wanapohitaji huduma mbalimbali kutoka kwenye ofisi hizo.

No comments: