Monday, September 14, 2015

WACHAFUZI WA MAZINGIRA MJI WA MBINGA KUPIGWA FAINI

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Simon Ngaga akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake vya kikazi wilayani humo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKAZI wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuuweka mji huo katika hali ya usafi wakati wote ili waweze kuepukana na magonjwa yanayoweza kutokea hapo baadaye, kutokana na taka kuzagaa ovyo.

Aidha kwa atakayekamatwa akionekana anachangia kuufanya mji huo uwe katika hali mbaya ya uchafu kwa kutupa taka katika maeneo ambayo sio rasmi, wamepewa onyo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya shilingi 50,000 pamoja na kufikishwa Mahakamani, ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Ofisa afya wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Felix Matembo alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusisitiza kuwa halmashauri hiyo, imejiwekea mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba suala hilo linapewa kipaumbele ili kuweza kuepukana na madhara yatakayoweza kuathiri jamii.


Matembo alifafanua kuwa katika kuhakikisha utekelezaji wake unaleta ufanisi, tayari kuna vibarua ambao wameingia mikataba ya muda na halmashauri hiyo wanafanya kazi ya ufagizi katika maeneo ya umma, kama vile masoko, stendi kuu ya abiria na kuzunguka barabara za mji huo.

“Hivi sasa kazi hii ya usafi tunaifanya wenyewe kwa kutumia vibarua ambao wanashughulika katika maeneo haya ya umma, mimi kama mtaalamu wa mambo ya usafi ninahakikisha taka zote zinatupwa kwenye maghuba na baadaye huzolewa na kuteketezwa kwenye dampo la kuhifadhia taka lililopo eneo la zamani la uwanja wa ndege”, alisema Matembo.

Ofisa afya huyo aliendelea kubainisha kuwa mkakati mwingine walionao katika kufanikisha hilo, kila wiki wamekuwa wakipita mtaani kwa kutumia gari la matangazo kuwatangazia wananchi wahakikishe wanazingatia kanuni za usafi.

Kadhalika aliongeza kuwa kwa kila mwezi, wiki ya kwanza siku ya Jumamosi baadhi ya viongozi wa mji huo kwa kushirikiana na wananchi wamekuwa wakitekeleza kwa vitendo katika maeneo ya kijamii, kwa kufanya usafi ikiwa ni lengo la kuhamasisha wananchi kuzingatia masuala hayo ya usafi.

Pamoja na mambo mengine, Matembo alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili ofisi yake na kusababisha wakati mwingine washindwe kumudu ipasavyo shughuli za usafi ni upungufu wa wataalamu, ambapo kwa sasa ofisi yake inao wawili tu na kwamba vitendea kazi kama vile magari ya kuzolea taka nalo limekuwa ni tatizo sugu kwao, wana gari moja tu ambalo halikidhi mahitaji husika.


Akizungumzia kwa upande wa mfumo wa maji taka katika mji wa Mbinga, alisema tayari serikali imeagiza gari la kunyonya maji hayo ambapo siku chache zijazo litawasili kwa ajili ya kufanya kazi hiyo, ili halmashauri yao ya mji iweze kuondokana na adha ya kukodi gari kutoka mbali kwa ajili ya kufanyia shughuli hiyo.

No comments: