Friday, September 4, 2015

NGONYANI: WALIOSHINDWA KWENYE MCHAKATO KURA ZA MAONI CCM TUACHE KUPAKANA MATOPE

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyefanikiwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kura za maoni, kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya chama hicho Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, Edwin Ngonyani amewasihi wanachama wenzake walioshindwa kwenye mchakato huo kuacha kupakana matope au kufikiria kukihama chama hicho, bali waungane pamoja ili kukipa nguvu na hatimaye kiweze kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Tabia na mawazo ya namna hiyo alieleza kuwa hayana mantiki yoyote ile, kwa kile alichodai kuwa hata kama watakimbilia kwenye vyama vingine vya siasa kwa lengo la kutafuta uongozi, bado nafsi zao zitawasuta.

Ngonyani aliyasema hayo muda mfupi mara baada ya msimamizi wa uchaguzi kura za maoni wilayani humo, Oscar Msigwa kumtangaza kuwa ndiye aliyeshinda kugombea nafasi hiyo ya ubunge katika jimbo hilo.


Aidha aliwashukuru wanaccm kwa kumchagua kwenye kinyang’anyiro hicho, ambapo hii ni mara ya pili kwake kugombea nafasi hiyo ya ubunge katika jimbo la Namtumbo, na kwamba mara ya kwanza aliwahi kugombea mwaka 2010 ambapo kura hazikutosha.

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni mwaka huu, alieleza amejifunza kwamba jambo kubwa aliloliona ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua na kukemewa ni pale wagombea wanapotumia nguvu kubwa ya kifedha kusaka madaraka, jambo ambalo linahatarisha kuwanyima haki wagombea ambao wanasifa ya kuongoza wananchi lakini hawana fedha ya kufanya hivyo.

Mchakato wa kura za maoni kwa nafasi ya ubunge kwenye jimbo hilo umelazimika kurudiwa mara tatu, ambapo kwa mara ya kwanza Vita Kawawa aliibuka mshindi ambapo matokeo yake yalipingwa na wagombea wenzake 11 kwa kile kilichodaiwa kuwa kuwepo kwa kasoro ya kuzidi kura zilizopigwa tofauti na idadi ya wanachama, ambao walistahili kupiga kura husika.

Kutokana na kasoro hiyo, Katibu Mkuu taifa wa CCM Abdulrhaman Kinana aliamuru kurudiwa kwa uchaguzi huo ambapo Ediwn Ngonyani aliibuka mshindi kwa kupata kura 12,606 huku nafasi ya pili, ikichukuliwa na Salome Sijaona kwa kupata kura 7,002 na Vita Kawawa akishika nafasi ya tatu kwa kuambulia kura 2,749.


Hata hivyo matokeo hayo yalilalamikiwa tena na wagombea wengine akiwemo, Kawawa ambapo hata uliporudiwa kwa mara ya tatu bado Ngonyani aliweza kuwashinda wagombea wenzake, kwa kupata kura 13,573 huku mpinzani wake wa karibu, Kawawa akipata kura 10,068 na Salome Sijaona kura 6,015.

No comments: