Monday, September 7, 2015

NALICHO NAMTUMBO AWATAKA WANASIASA KUTOKUWA CHANZO CHA VURUGU

Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

WAKATI joto la uchaguzi likiendelea kupanda kwa vyama vya siasa na wagombea wake ndani ya vyama hivyo, imeshauriwa kuwa ni vyema wagombea hao wajenge moyo wa subira na uvumilivu juu ya mambo yanayohusiana na maslahi ya taifa, ikiwemo kutoa nafasi kwa wananchi kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo na sio kuwa chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini na wagombea nafasi mbalimbali za uongozi katika vyama vya siasa, wilayani humo.

Nalicho alisema kuwa suala la maslahi ya kitaifa ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele, na wanasiasa kuacha kutanguliza maslahi yao binafasi ili waweze kuwatumikia vyema Watanzania.


Aidha aliwataka viongozi wa dini wilayani Namtumbo, kuhakikisha wanawahimiza waumini wao kushiriki vyema kwenye uchaguzi mkuu na kujiepusha kumchagua mtu kwa misingi ya itikadi ya dini au kabila.

“Viongozi wenzangu nawaombeni sana kuelimisha waumini wetu kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu mwaka huu, wananchi wasikose kushiriki kwenye mikutano ya kampeni ya vyama vyote vya siasa kwani hii ndiyo fursa pekee ya kuwapima wagombea wetu kama wanafaa au hawafai, ili baadaye tuweze kumchagua kiongozi bora wa kuweza kuongoza taifa letu”, alisema Nalicho.

Kadhalika alisema suala la uchaguzi si la mtu mmoja au chama fulani cha kisiasa bali ni kwa ajili ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura, hivyo kuna umuhimu kwa viongozi wa vyama hivyo wanapopanda majukwaani na viongozi wa dini wanapokuwa kwenye nyumba za ibada kuhubiri amani, ili uchaguzi huo ufanyike kwa utulivu.


Kila mtanzania kwa nafasi aliyonayo alisema, anapaswa kuimba wimbo huo na kujiepusha kueneza maneno yanayoweza kusababisha kuleta chuki na vurugu kwa wafuasi wa chama kimoja au kingine, kwa kile alichoeleza kuwa watanzania wengi wanapenda kuendelea kuishi na kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

No comments: