Thursday, September 24, 2015

MGONJWA AMSHAMBULIA KWA KIPIGO MUUGUZI WA HOSPITALI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mgonjwa ambaye alikuwa amelazwa Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mariam Njaidi amezua jambo baada ya kumshambulia kwa kipigo Muuguzi mmoja wa kitengo cha maabara katika hospitali hiyo, kutokana na kucheleweshewa majibu ya vipimo vyake vya magonjwa ya taifodi na sukari.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Thabit Mwambungu.
Mgonjwa huyo ambaye alikuwa amelazwa wodi namba tatu, aliwashangaza wagonjwa wenzake waliolazwa hospitalini hapo baada ya kuamka kitandani alipokuwa amelala na kwenda kumfuata muuguzi, Hiren Msokwa katika chumba cha maabara na kuanzisha mapigano kati yao ambaye baadaye alimkuta akiwa na majibu yake mikononi mwake.

Hali hiyo inadaiwa ilitokana na Njaidi kucheleweshewa majibu ya vipimo vya magonjwa hayo kwa zaidi ya siku tatu, ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.


Mashuhuda wa tukio hilo walisema, awali mabishano yalianza kutokea kati ya wauguzi waliokuwa zamu katika wodi hiyo na mgonjwa huyo ndipo alipochukua maamuzi ya kwenda mwenyewe, kufuata majibu ya vipimo vyake maabara ambako alikutana na muuguzi huyo na kuanza kupigana naye.

Pamoja na mambo mengine, uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa matatizo hayo katika hospitali ya Tunduru yanatokana pia na baadhi ya wafanyakazi wake kutotimiza majukumu ya kazi zao ipasavyo, ndio maana kumekuwa na migongano kati yao na wagonjwa.

Nimezungumza kwa nyakati tofauti na baadhi ya wagonjwa wanaokwenda kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo, walidai kuwa jambo hilo limekuwa ni tatizo sugu linaloendelea kuwatesa pale wanapohitaji matibabu hospitalini hapo, na kwamba wanaiomba serikali kuingilia kati ili kuweza kunusuru hali hiyo.

Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dokta Zabron Mmari alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mapigano hayo yalisababisha, Msokwa kupatwa na majeraha ya kawaida mwilini.


Alisema hali hiyo inatokana na kujirudia matukio ya aina hiyo, ambapo Septemba 16 mwaka huu mlinzi wa hospitali hiyo, Chande Bakari naye alivamiwa na ndugu ya mtunza mgonjwa aliyekuwa hospitalini hapo ambaye alifahamika kwa jina la, Jobe Khatibu.

No comments: