Tuesday, August 22, 2017

DC AKEMEA VITUO VYA AFYA WILAYA YA MBINGA KUKOSA DAWA

Upande wa kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye akiwataka watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo kutekeleza majukumu waliyopewa na serikali kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa, kushoto ni Mkurugenzi mtendaji Gombo Samandito na katikati ni Mwenyekiti wake wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Ambrose Nchimbi.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba ni aibu kuona au kuendelea kusikia katika zahanati na vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo wilayani humo, kwamba fedha zipo za kununulia dawa lakini wagonjwa wanalalamika hakuna dawa.

Nshenye alisema kuwa hivi karibuni alitembelea katika baadhi ya vituo hivyo wilayani hapa na kukuta malalamiko hayo ambapo kufuatia hali hiyo ameagiza kuwa endapo itaendelea sasa utafika wakati wa wahusika kuwajibishwa pale atakapoona kuna tatizo kama hilo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo wakati alipokuwa akihutubia katika kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani humo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.


Alisema kuwa panapotokea hakuna dawa katika vituo hivyo vya afya sio tatizo la serikali ni tatizo na uzembe wa watendaji wa kada hiyo, kwani fedha za kununulia dawa hizo zinakuwepo ila kunakuwa na uchelewaji wa kuziagiza kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD) iliyopo hapa nchini.

“Nimefanya ziara ya kutembelea vituo hivi, lakini vingi vilikuwa havina dawa kwa hiyo nirudie kusema panapotokea hakuna dawa sio tatizo la serikali ni tatizo la watendaji wetu tutaendelea kushughulikia hili na kushughulika nao”, alisisitiza Nshenye.

Kadhalika Nshenye aliwataka viongozi ndani ya wilaya hiyo wajipange sasa katika jukumu la kuongeza ujenzi wa vituo vya afya ili kuweza kusogeza huduma karibu na wananchi.


Hata hivyo alisisitiza kuwa katika ujenzi huo wahakikishe kwamba kwa mujibu wa sera ya afya ndani ya vituo hivyo wanajenga chumba cha upasuaji na wodi za kulaza wagonjwa hasa ikilenga kuweza kutoa huduma karibu na akina mama wajawazito ambao wanaishi mbali na hospitali ya wilaya.

No comments: