Tuesday, August 29, 2017

WAKULIMA WA SOYA WAKABILIWA NA CHANGAMOTO LUKUKI

Na Mwandishi wetu,      
Songea.

MKOA wa Ruvuma umetajwa kuwa ni miongoni mwa mikoa michache hapa nchini ambayo inazalisha zao la Soya kwa wingi, huku changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa soko la uhakika licha ya uzalishaji wake kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Dokta Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akifungua kikao cha Wadau wa zao hilo ambacho kilijumuisha mikoa mitatu ya Ruvuma, Iringa na Njombe kilichofanyika katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.

Alisema uzalishaji wa Soya umekuwa ukiongezeka toka msimu wa 2014/2015 na msimu wa mwaka 2016/2017 ambapo ulizalisha hekta 33,267 zilizoweza kutoa tani 32,331 ukilinganisha na msimu wa mwaka 2015/2016 ambao kulikuwa na hekta 19,026 zilizotoa tani 16,754.


Hilo ni ongezeko la ukubwa wa hekta 14,241 na uzalishaji wa tani 15,577 sawa na ongezeko la asilimia 48 ya uzalishaji kwa msimu wa 2015/2016 ambalo linaonesha jinsi gani wakulima wa mkoa huo walivyohamasika kulima zao hilo.

Dokta Mahenge alifafanua kuwa changamoto kubwa inayowakabili wakulima hao ni soko la kuuzia zao hilo ambapo hivi sasa kuna kampuni moja ya Silverlands ambayo hupita kununua kupitia wakulima waliopo kwenye vikundi huku mkulima mmoja mmoja akiuza kwa kampuni binafsi ya Export Trade Company Limited.

Aliongeza kuwa tatizo kubwa lingine wanalokabiliana nalo wakulima hao mazao yao kutonunuliwa kwa wakati baada ya kuyakusanya kwenye maghala ambako wanayahifadhi.

Kwa upande wake mwakilishi wa mpango wa kuendeleza kilimo cha mazao mbalimbali katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (Sagcot) Maria Jumba alisema kuwa kuna maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo katika ukanda wa mikoa ya nyanda za juu kusini ikiwemo Ruvuma.

Hivyo basi alisema kuwa kazi kubwa ya Sagcot ni kuratibu malengo mahususi ili kuweza kuleta tija kupitia shughuli za kilimo katika ukanda fulani na kutoa kushauri kwa wakulima ili kuongezeka uzalishaji hasa baada ya soko la Tanzania kufunguka na kuwepo kwa makubaliano ya kibiashara na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maria aliwaasa Watanzania kutoogopa ushindani wa kibiashara badala yake kutumia fursa iliyopo kujikita zaidi kwa kuzalisha bidhaa bora zitakazoweza kuingia katika soko la ushindani.

No comments: