Wednesday, August 2, 2017

RC RUVUMA ATOA ONYO KWA WAKURUGENZI WATENDAJI NA WAKUU WA IDARA KATIKA HALMASHAURI ZA WILAYA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge upande wa kushoto akiangalia sabuni aina ya magadi iliyotengenezwa na Wajasirimali wadogo kutoka wilaya ya Tunduru mkoani humo alipotembelea na kukagua mabanda ya bidhaa za kilimo katika eneo la nanenane Manispaa ya Songea mjini hapa jana.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge wa pili upande wa kulia akiangalia bustani ndogo ya kilimo cha Karoti inayotumika kufundishia wakulima katika maonesho ya wakulima nanenane mkoani humo jana, wa pili kulia ni Afisa kilimo wa kata ya Sisi kwa Sisi kutoka halmashauri ya wilaya ya Tunduru Lucy Komba na wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Abdallah Mussa.
Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amepiga marufuku kwa kuwataka Wakurugenzi na Wakuu wa idara katika halmashauri za wilaya mkoani humo, kuacha mara moja tabia ya kuhamisha na kubadili matumizi ya fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi ikiwemo kilimo na miradi mingine.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu huyo wa mkoa jana wakati akizungumza na wakulima, watendaji wa serikali pamoja na wananchi waliohudhuria ufunguzi wa maonesho ya wakulima nanenane ambayo kimkoa yanafanyika katika viwanja vya nanenane vilivyopo katika kata ya Msamala Manispaa ya Songea mjini hapa.

Dokta Mahenge alisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikikwamisha mkakati wa kuinua maendeleo ya wananchi hasa kwa upande wa shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali, kwa sababu baadhi ya wakuu hao wa idara hushirikiana na wakurugenzi wao kuiba fedha hizo kwa mtindo huo jambo ambalo linarudisha nyuma mpango wa kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.


Alisisitiza kuwa suala la kuongeza tija katika uzalishaji kwa eneo ni muhimu na kama tunataka kujitosheleza kwa chakula na kupata ziada ya kuuza nje ya nchi ni muhimu kuongeza kiwango cha uzalishaji na sio vinginevyo.

Vilevile alibainisha kuwa takwimu za uzalishaji wa zao la mahindi katika mkoa wa Ruvuma zinaonesha kwamba hekta moja inazalisha kati ya tani 2 hadi 3 lakini utafiti unathibitisha kuwa hekta hiyo moja inaweza kuzalisha hadi kufikia tani 7 hivyo mkulima anapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili aweze kufikia malengo hayo.

Kutokana na hali hiyo Dokta Mahenge amewataka wakulima wa mkoa huo waachane na tabia ya kilimo cha mazoea ambacho katika kipindi cha msimu wa uzalishaji wa mazao ya chakula mkoani humo kimekuwa kikiwarudisha nyuma licha ya kazi kubwa wanayoifanya mwaka hadi mwaka.

Alisema mkoa una eneo la ukubwa wa hekta 59,943 linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini hadi sasa eneo linalotumika ni hekta 10,266.1 tu sawa na asilimia 17 ya eneo hilo licha ya kilimo hicho kuwa ndiyo mhimili mkubwa wa kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali.

Pia amezitaka halmashauri za wilaya kwa kushirikana na wananchi ziendelee kuomba fedha za ujenzi wa skimu za umwagiliaji kupitia mfuko wa umwagiliaji wa wilaya (DIDF) chini ya programu ya kuendeleza sekta ya kilimo ili kuweza kujenga na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji iliyopo mkoani hapa.

Kadhalika takwimu za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara katika mkoa huo zinaonesha kuwa katika msimu wa mwaka 2016/2017 jumla ya hekta 837,208 za mazao ya chakula na biashara ambazo zilitoa mavuno tani 1,858,908 wakati mahitaji ya chakula kwa wakazi wa mkoa huo wapatao 1,376,891 kulingana na sensa ya mwaka 2012 ni tani 469,172 kwa mwaka na huku ziada ya chakula ikiwa ni tani 1,689,699 za mazao ya chakula.

Pamoja na mambo mengine aliwapongeza wananchi kwa mafanikio hayo yaliyofikiwa kwani chakula cha ziada kilichozalishwa kitasaidia kulisha wananchi katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa chakula hapa nchini na ziada kuuzwa licha ya hivi sasa kukabiliwa na changamoto nyingi katika uzalishaji, uhifadhi, usindikaji na masoko.

Aliwataka wakulima wa  mazao ya kahawa, tumbaku na korosho kuwa tayari kutumia mikutano ya wadau katika kupanga mikakati ya kujadili hali ya masoko ipoje, sambamba na wataalamu wa kilimo na mifugo kuwa na tabia ya kuwafikia wakulima na kutoa huduma za ugani kwa wakati ili kuongeza tija ya uzalishaji kwa mazao ya kilimo na mifugo.

Awali Katibu tawala msaidizi wa mkoa huo Bwai Biseko alisema kuwa maonesho hayo ya nanenane mwaka huu yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya, ambapo lengo lake wananchi watumie fursa ya maonesho hayo kwa ajili ya kuona na kujifunza kwa lengo la kuchochea maendeleo katika sekta hiyo muhimu.


Hata hivyo mkakati wa serikali ya awamu ya tano ni kukifanya kilimo kuwa ndiyo njia kuu ya kukuza uchumi ambapo wananchi wenyewe ni washiriki wakuu katika maonesho hayo.

No comments: