Sunday, August 27, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKUTANA NA MAKAMU WA RAIS WA CUBA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NAYE

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya mazungumzo ya kikazi na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano katika mji wa Havana nchini Cuba jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Na Mwandishi wetu,

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano na kumhakikishia ufunguzi wa Ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Aidha Majaliwa alisema kuwa Tanzania inatambua na kuthamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kiafya na kiutamaduni kati yake na Cuba hivyo inatarajia kufungua ubalozi nchini humo ili kuweza kurahisisha utendaji wa kazi za kibalozi.

Waziri Mkuu huyo alikutana na Makamu huyo wa Rais jana wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Cuba ambapo malengo ya ziara hiyo yalikuwa ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.


“Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati Tanzania na Cuba ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, hivyo lazima tufungue ofisi za ubalozi na tutamleta balozi wetu hapa”, alisema.

Pia aliishukuru Serikali ya Cuba kwa ujenzi wa kiwanda cha dawa za kuua vijidudu vya maralia pamoja na ufadhili wa masomo ya udaktari inaoutoa kwa wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali nchini humo.

Vilevile aliiomba Serikali hiyo iendelee kutoa ufadhili wa masomo kwa madaktari hao hadi ngazi ya shahada ya uzamili kwa sababu Serikali ya Tanzania inawahitaji madaktari bingwa wengi kwani waliopo sasa ni wachache.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Gladys alimshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kufanya ziara nchini Cuba na kumhakikishia kwamba uhusiano wa Serikali yake na ya Tanzania utaendelea kuimarishwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Alisema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dokta John Magufuli inafanya jitihada kubwa ya kuhakikisha uchumi wake unakua kwa kasi jambo ambalo ni tofauti na mataifa mengine.


Makamu huyo wa Rais aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana katika uboreshaji wa Sekta ya afya, utamaduni, kilimo, uchumi na elimu na kwamba kuhusiana na ombi la kuongeza ufadhili wa shahada ya uzamili kwa madaktari alisema alilipokea na kueleza kuwa atalifanyia kazi.

No comments: