Wednesday, August 2, 2017

MKEMIA MKUU: MKOJO WA MASOGANGE UMEBAINIKA KUWA NA HEROIN

Na Mwandishi wetu,

MKEMIA kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali, Elias Mulima ameiambia Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu kuwa sampuli ya mkojo wa msanii Agnes Gerald maarufu kama Deal ama Masogange (28) umebainika kuwa na dawa ya kulevya aina ya Heroin.

Akitoa ushahidi huo leo Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka akiongozwa na Wakili wa serikali, Constantine Kakula alisema kuwa February 15 mwaka huu askari wawili kutoka Jeshi la Polisi hapa nchini Koplo Sospeter na WP Judith, walimfikisha Masogange ofisini kwake kwa lengo la kumfanyia vipimo vya mkojo wake.

Agness Masogange.
Baada ya kuwapokea, alimsajili Masogange na kumpa namba ya maabara 446/2017 na kisha kuwakabidhi kifaa maalum kwa ajili ya kuweka sampuli hizo za mkojo.

Alidai baada ya kupokea sampuli hizo, Masogange alifanyiwa uchunguzi kwa kutumia kemikali na kubaini kuwa mkojo wake una chembechembe za dawa za kulevya aina ya Heroin ambazo kwa kitaalamu zinajulikana kama Diacety Imophine.

Kadhalika uchunguzi zaidi unaeleza na kufafanua kuwa chembechembe hizo za dawa nyingine ya kulevya ni aina ya Oxazepam.


Shahidi huyo alidai kuwa baada ya kufanya uchunguzi huo aliandaa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na sampuli hiyo ya mkojo ambapo aliisaini yeye mwenyewe na kuthibitishwa juu ya madawa hayo ya kulevya na kwamba shahidi huyo alimtambua Masogange kuwa ndiye aliyepelekwa kuchukuliwa sampuli hiyo ya mkojo ofisini kwake.

Vilevile alidai kuwa anaweza kuitambua taarifa hiyo ya uchunguzi kutokana na kuwepo kwa saini yake, muhuri wa moto wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali ambapo ameomba Mahakama kupokea vitu hivyo kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.

Mawakili Nehemiah Nkoko na Reuben Simwanza ambao wanamtetea Masogange wamepinga taarifa hiyo ya uchunguzi wakitaka isipokelewe na Mahakama hiyo kwa madai kwamba haijakidhi vigezo vya kisheria.

Nkoko alidai kuwa utaratibu wa kisheria haukufuatwa kabla ya mtuhumiwa alipokuwa chini ya Polisi kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, kwa kuwa ofisa wa Polisi alitakiwa kuwasilisha maombi Mahakamani ndipo amri ya kupimwa itolewe.

“Ripoti ipo kinyume na sheria Mahakama ina njia moja tu nayo ni kuikataa na sio kuikubali, sheria ipo wazi tunaomba Mahakama ikubali pingamizi letu na kukataa kupokea taarifa hiyo”, alisisitiza.

Naye Wakili Simwanza alidai ripoti hiyo ikitazamwa inataja fomu nyingine ya ombi la Jeshi la Polisi kwenda kwa Mkemia mkuu kwa ajili ya kufanya vipimo huku akidai kuwa ripoti hiyo ipo yenyewe bila ya kuambatanishwa na fomu maalum inayotumiwa na Polisi kupeleka sampuli hivyo haiwezi kupokelewa na kutumika kama kielelezo.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kakula alidai pingamizi hilo halina mashiko wala miguu ya kusimamia kwani fomu ambayo haijaambatanishwa na ile ya mkemia mkuu ni vitu viwili tofauti na hata uwasilishwaji wake unafanywa na watu wawili tofauti.

Kaukala alifafanua kuwa taarifa ya mkemia inawasilishwa na mkemia na ile ya Polisi inawasilishwa na Polisi ambapo kuhusu hoja ya sampuli ya mkojo, Wakili huyo alidai kuwa kifungu cha 63 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA), kimeweka mazingira ambayo ofisa wa Polisi atawasilisha maombi Mahakamani kuweza kuchukua sampuli.

Pamoja na mambo mengine endapo mtuhumiwa anakataa kuchukuliwa sampuli ya mkojo, hivyo atawasilisha ombi Mahakamani ili iweze kutolewa amri, hivyo Kakula alisema katika pingamizi lao upande wa utetezi haujaeleza kwamba mshitakiwa alikataa kupima au alilazimishwa na kwamba aliomba pingamizi hizo zitupiliwe mbali.


Hakimu Mashauri aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 28 mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa kupokelewa kwa taarifa hiyo au la, Masogange amefikishwa Mahakamani hapo akidaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin kati ya Februari 7 na 14 mwaka huu katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jiji  la Dar es Salaam hata hivyo yupo nje kwa dhamana.

No comments: