Friday, August 18, 2017

IDARA ZA SERIKALI MANISPAA SONGEA ZAINGIA KATIKA KASHFA NZITO

Mhasibu wa Mamlaka ya Maji safi na Uhifadhi Mazingira (SOUWASA) Leonard Luhagila akiwaonesha baadhi ya Waandishi wa habari mitambo mipya ya kusukumia maji katika chanzo cha mto Luhira katika Manispaa ya Songea jana ambapo gharama za uendeshaji wake kwa mwezi ni kati ya shilingi milioni 20 hadi 25.
Na Mwandishi wetu,       
Songea.

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (SOUWASA) katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, inazidai baadhi ya taasisi na idara za serikali fedha zaidi ya shilingi milioni 794,118,058.38 ikiwa ni malimbikizo ya ankra ya maji hadi kufikia Julai 30 mwaka huu baada ya kusambaza huduma ya maji kwa taasisi hizo.

Aidha licha ya mamlaka hiyo kutoa notisi kwa idara na taasisi hizo ikizitaka kulipa deni hilo kuanzia Juni 28 mwaka huu hali imekuwa kinyume na kwamba ni taasisi mbili tu ambazo ni shule ya sekondari ya wasichana Songea iliyopo mjini hapa iliyokuwa inadaiwa shilingi 6,295,128.00 ambayo imelipa deni lake kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Chuo cha waganga wasaidizi Songea ambacho kimepunguza shilingi milioni 10 kati ya shilingi milioni 30,209,469.22 ambazo kilikuwa kinadaiwa.

Kaimu Mkurugenzi wa SOUWASA Mhandisi John Kapinga alisema kuwa Hospitali ya rufaa Songea ndiyo inayoongoza kwa kudaiwa shilingi milioni 276,233,440.73, ikifuatiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) shilingi 126,690,090.10, Magereza ya mkoa shilingi 153,594,369.55 na Polisi inayodaiwa shilingi 101,229,537.40.


Alizitaja taasisi nyingine kuwa ni shule ya Wavulana Songea shilingi 4,916,661.60 Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Songea shilingi 4,340,451.92, Manispaa ya Songea shilingi 6,574,868.79 Ofisi ya Katibu tawala mkoa wa Ruvuma (RAS) shilingi 51,306,330.27, Chuo cha Ualimu Songea (TTC) shilingi 12,852,690.00, shule ya sekondari London shilingi 12,920,563.50 na idara ya Maliasili inadaiwa shilingi 1,452,279.60.

Idara ya uhamiaji inayodaiwa jumla ya shilingi milioni 5,502,177.70 ambayo hivi sasa imekwisha katiwa huduma ya maji tangu mwezi Februari mwaka huu ambapo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge ameiomba Mamlaka hiyo kurejesha huduma ya maji kwa kuwa juhudi za kulipa deni hilo zinaendelea na Ofisi ya uhamiaji makao makuu Jijini Dar es Salaam.

Dokta Mahenge amewaagiza Wakuu wa idara hizo kwenda kusimamia ipasavyo matumizi ya maji na ikiwezekana kufunga mita za maji ili kuepusha matumizi makubwa ya upotevu wa maji usiokuwa wa lazima katika taasisi zao.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa ni lazima idara na taasisi hizo zilipe madeni hayo kwa wakati ili kuweza kuifanya Mamlaka hiyo ya maji kuzalisha maji kwa wingi ambayo asilimia kubwa uzalishaji wake umekuwa ukifanywa kwa kusukumwa na mashine zinazotumia nishati ya umeme katika kutoa huduma husika kwa wananchi.

Alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona licha ya SOUWASA ikijitahidi kuboresha huduma zake, lakini taasisi hizo za umma hazilipi ankra za maji kwa wakati badala yake zimekuwa zikilimbikiza madeni yao kwa muda mrefu na kufikia hatua ya kuwa makubwa.


Hata hivyo kwa upande wake Mhasibu wa Mamlaka hiyo ya maji, Leonard Luhagila alifafanua kuwa gharama ya kuendesha mitambo ya kusukuma na kuzalisha maji kwa nguvu ya umeme, kwa mwezi ni kati ya shilingi milioni 20 hadi 25 na kwamba hivi sasa mamlaka imekuwa ikidaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma zaidi ya shilingi milioni 30.

No comments: