Saturday, August 19, 2017

MADIWANI WAMWAJIBISHA MHANDISI IDARA YA MAJI MBINGA

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, wakisikiliza kwa makini maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao chao cha baraza la Madiwani kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbinga, Ambrose Nchimbi akitangaza maamuzi yaliyochukuliwa na baraza la Madiwani wake dhidi ya Mhandisi wa idara ya maji wa halmashauri hiyo Vivian Mndolwa mara baada ya kuketi juzi katika kikao cha baraza la Madiwani kupitia kamati yake ya mamlaka ya nidhamu, upande wa kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Gombo Samandito.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imemrejesha kazini Mhandisi wa idara ya maji wilayani humo Vivian Mndolwa huku akipewa adhabu ya kukatwa na kupokea nusu ya sehemu ya mshahara wake katika kipindi cha mwaka mmoja.

Adhabu hiyo imetolewa juzi na baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo katika kikao chao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa ambapo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambrose Nchimbi alisema hayo mbele ya baraza hilo mara baada ya kuketi kikao cha kamati ya mamlaka ya nidhamu kwa muda wa zaidi ya masaa matatu na kufikia muafaka wa kutoa adhabu hiyo.

Nchimbi alisema kuwa utekelezaji wa adhabu hiyo unaanza mapema kuanzia sasa mwezi Agosti mwaka huu na kwamba inafuatia baada ya Mhandisi huyo kupatikana na tuhuma ya kushindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa mradi wa maji uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja, kijiji cha Mkako kata ya Mkako ambao unadaiwa kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji ipasavyo wananchi katika maeneo husika ndani ya kata hiyo.


Aidha Mndolwa hapo awali alisimamishwa kazi kufuatia agizo lililotolewa Mei 8 mwaka huu na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour kwa kumtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kuunda kamati ambayo ilifanya kazi ya kuchunguza tatizo hilo na baadaye hatua husika ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika waliohujumu mradi huo.

Pia mradi huo imeelezwa kuwa ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 718,896,533 chini ya ufadhili wa benki ya dunia ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike katika kipindi cha mwaka mmoja tangu uanze kujengwa, lakini hadi kufikia kipindi cha mwaka huu 2017 ujenzi huo bado haujakamilika na fedha za mradi huo zimetumika katika kazi hiyo ya ujenzi.

Vilevile kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imeelezwa kuwa ni ya PATTY Interplan ya kutoka Jijini Dar es Salaam na kwamba tayari halmashauri ya wilaya hiyo imevunja mkataba na mkandarasi huyo baada ya kuonekana kumekuwa na ubabaishaji mkubwa juu ya ukamilishaji wa ujenzi wa mradi huo.

Mpaka sasa hatua ya ujenzi wa mradi huo yamejengwa matenki mawili ya maji ikiwemo moja kubwa lenye ujazo wa lita 200,000 na lingine ndogo lenye ujazo wa lita 75,000 ikiwemo ufukiaji chini wa mabomba ya Plastiki kutoka kwenye chanzo kikuu cha kuleta maji katika matenki hayo.

Kadhalika vituo 36 vya kuchotea maji vimejengwa lakini kutokana na ucheleweshaji wa ujenzi wa mradi huo na kuleta maji kwenye mabomba hayo kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa kata ya Mkako wilayani Mbinga, inadaiwa kuwa siku kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru alipowasili hapo walipojaribu kuleta maji kwenye matenki hayo kwa ajili ya kupeleka kwenye vituo hivyo vya kuchotea maji, mabomba hayo yalikuwa yamepasuka na kushindwa kupeleka maji katika vituo hivyo jambo ambalo linadhihirisha wazi kuwa ujenzi wa mradi huo ulikuwa ni wa chini ya kiwango.


Hivyo basi, Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga iliunda Kamati maalumu ya watu saba ambayo ndiyo ilichunguza suala hilo ambayo ilitoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya wilaya na wengine walikuwa ni wajumbe wa ngazi ya halmashauri ya wilaya hiyo na kubaini kwamba ujenzi wake ulifanyika chini ya kiwango.

No comments: