Thursday, August 10, 2017

MAKALA: MAMLAKA YA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MBINGA NA MIKAKATI YA KUBORESHA HUDUMA ZAKE


Pichani ni tanki kubwa la maji ambalo limejengwa na Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) mji wa Mbinga mkoani Ruvuma ambapo hivi karibuni, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour alikagua mradi huo na kuufungua tayari kwa kuanza matumizi kwa wakazi wa mji huo na kwamba tayari tanki hilo limekuwa likitumika kusambaza maji kwa wakazi wa mji wa Mbinga.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour akiwa amepanda juu ya tanki hilo kubwa la maji ambalo limejengwa na Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuukagua mradi huo ambapo kiongozi huyo wa mbio za Mwenge alipongeza ujenzi huo umefanyika kwa ubora unaotakiwa na kwamba hivi sasa tayari tanki hilo limekuwa likitumika kusambaza maji kwa wakazi wa mji huo. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,

UMUHIMU wa maji katika maisha ya binadamu au kiumbe chochote kile kilichokuwa hai hapa duniani ni jambo ambalo halina mjadala, kutokana na hilo ndio maana serikali mara zote imekuwa ikihimiza umuhimu wa kutunza mazingira ili kunusuru vyanzo vya maji vilivyopo viweze kuwa endelevu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Tatizo la kukosekana kwa maji linaweza kusababisha matatizo mengi katika jamii ikiwemo kutokea kwa magonjwa ya mlipuko na maji  hayo endapo yanapatikana kwa shida, hugeuka na kuwa karaha  hasa kwa akinamama ambao ndio watu wanaohusika kwa kiasi kikubwa kuyatafuta.

Baada ya kuona umuhimu huo, serikali imeamua kuanzisha Mamlaka za maji ambazo zimekuwa zikisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo ya miji.

Halmashauri ya mji wa Mbinga iliyopo mkoani Ruvuma, kuna Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) ambayo hivi sasa imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mji huo, katika kuendeleza huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mwandishi wa makala haya kwa kushirikiana na vyanzo mbalimbali vya habari amebaini kuwa katika mji huo kumekuwa na vyanzo sita vya maji, ambavyo vimeainishwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi ili waweze kuondokana na tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.


Kwa mujibu wa taarifa ya maendeleo ya utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa mji wa Mbinga inafafanuliwa kuwa, mkakati uliopo sasa ni kuongeza na kuboresha vyanzo vya uzalishaji maji vilivyopo kutokana na hitaji la maji katika mji huo kuwa kubwa.

Chanzo kilichopo sasa ambacho kinatumika katika kuzalisha nishati hiyo muhimu ni kimoja tu ambacho ni cha Ndengu, hakitoshelezi hitaji hilo la maji hivyo mikakati imewekwa ili kuondoa tatizo hilo sugu na kwamba tayari ujenzi wa miundo mbinu mipya ya maji yaani vyanzo vingine vinne vya Lupembe umeanza kufanyika ikiwemo tenki moja kubwa la kupunguza msongo wa maji na matenki madogo manne ya kukusanyia maji, ambapo katika kipindi cha miezi mitatu kazi hiyo imeelezwa kwamba itakuwa ujenzi wake umekamilika.

Pamoja na ujenzi huo kuendelea kufanyika pia uchimbaji wa mitaro nayo inajengwa kwa ajili ya kuweza kufukia mabomba makubwa yatakayoleta maji kwa wingi zaidi katika mji huo.

Meneja wa MBIUWASA, Patrick Ndunguru akizungumzia hilo anaeleza kuwa changamoto kubwa waliyonayo sasa ni uchakavu wa miundombinu ya kuleta maji hayo kutoka kwenye chanzo cha Ndengu hadi Mbinga mjini, ambapo miundombinu yake ni ya zamani imejengwa mwaka 1970 hivyo imekuwa ikisababisha upotevu mkubwa wa maji ambayo yanapaswa kuwafikia walaji.

Ndunguru anafafanua kuwa hayo yote yanatokana na uwezo mdogo wa uzalishaji maji unaosababishwa na kupanuka kwa mji, unahitaji kupanuliwa kwa miundombinu hiyo haraka, kwani uzalishaji uliopo sasa ni mita za ujazo 2,100 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji halisi yanayohitajika ni mita za ujazo 5,248.

Aidha anabainisha kuwa katika kuendeleza na kuboresha huduma hiyo muhimu anaishukuru Serikali, kupitia Wizara ya maji na umwagiliaji imetenga shilingi Bilioni 1 katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ambazo zitawezesha kupanua bomba kuu la uzalishaji maji hivyo kumudu ongezeko kubwa la mahitaji ya maji kufika katika eneo la mji.

“Vilevile Wizara imekuwa ikitoa fedha kwa awamu kwa lengo la kuweza kukamilisha mradi huu mkubwa ambao tumeanza kuujenga hapa lengo kuu ni kuongeza uwingi wa maji, katika mwaka 2017 hadi 2018 malengo yetu pia ni kujenga machujio ambayo kazi yake kubwa ni kutibu maji kabla hayajasafirishwa kwenda kwa watumiaji”, alisema Ndunguru.

Anaongeza kuwa mradi huo unalenga kupanua huduma kwa kuyafikisha maji katika maeneo mengine ya mji huo ambayo hayajafikiwa na huduma ambapo ujenzi wake utakuwa unatekelezwa kwa awamu, kulingana na kiasi cha fedha watakachokuwa wanapata hivyo anaiomba serikali kupitia wizara husika iendelee kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu hiyo ili mradi uweze kukamilika ujenzi wake.

Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira katika mji huo wa Mbinga kwa ujumla ilianza kazi yake rasmi Septemba Mosi mwaka 2003 ambapo tokea kuanzishwa kwake mpaka sasa ina jumla ya wateja 2,426 ambao wameunganishiwa maji na kufungiwa mita.

Hivyo basi, eneo hilo la mji lina jumla ya wakazi 59,655 kati ya hao 27,501 wanaishi kwenye eneo la mtandao wa bomba la maji hayo safi na salama ambapo ni sawa na asilimia 46.1 huku uzalishaji wa maji ukiwa ni mita za ujazo 58,967 kwa mwezi, ambapo maji yanayopotea kutokana na uchakavu wa miundombinu hiyo yanakadiriwa kuwa ni mita za ujazo 17,191 sawa na asilimia 29.2.

Katika kupambana na tatizo hilo ndio maana Wizara ya maji na umwagiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka hiyo, imeanza sasa kuboresha miundombinu ambayo ni chakavu ili kuweza kuondokana na changamoto hii ambayo imedumu kwa miaka mingi sasa.

Ndunguru anaeleza kuwa changamoto nyingine iliyopo mbele yao ni pamoja na baadhi ya wateja kutolipia ankra zao za maji kwa wakati, hivyo kuifanya mamlaka ishindwe kutekeleza majukumu yake ipasavyo ambapo anatoa wito kwa wateja wote waliopo ndani ya mji wa Mbinga ambao wameunganishiwa huduma hiyo ya maji walipe ankra hizo ili mamlaka iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Anasema tahadhari iliyopo sasa kwa wananchi ni kwamba wajiepushe na vitendo vya wizi wa maji kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha maendeleo ya mradi hivyo anaonya pia kwa watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa maoni yangu, sote tunatambua kuwa maji ni muhimu kwa maisha yetu ya kila siku hivyo kinachotakiwa kwa jamii ni kushiriki kikamilifu kuhakikisha vyanzo vinavyozalisha maji hayo vinatunzwa vizuri ili visikauke na kwamba njia mojawapo ya kuvitunza ni kuacha tabia ya kuchoma moto misitu, kulima karibu na vyanzo hivyo au kulisha mifugo na kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa chanzo cha maji kilichopo jirani naye.

Imekuwa ikisisitizwa mara tunapoona kuna tatizo katika eneo jirani la uharibifu wa mazingira tusisite kutoa taarifa katika mamlaka husika na viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza eneo ambalo uharibifu huo umetokea, wanalojukumu pia la kuhakikisha kwamba kila wanapofanya mikutano nao wasisite kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira hayo na vyanzo vya maji ambapo tukifanya hivi tutaweza kuondokana na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama.

No comments: