Wednesday, August 2, 2017

MTO LUNYERE DARPORI UNAKIWANGO KIKUBWA CHA KEMIKALI AMBAZO NI HATARI KWA VIUMBE HAI

Wachimbaji wa madini wakiwa katika mto Lunyere Darpori wakisafisha mchanga wenye madini.
Hili ni eneo moja wapo la mto Lunyere Darpori ambalo tayari limeharibiwa na wachimbaji hao.
Na Kassian Nyandindi,      
Nyasa.

TAASISI ya maji ya Water Laboratory unity na Chemical and Environmental services za Jijini Dar es Salaam, wamebaini kuwa mto wa Lunyere uliopo katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma una kiwango kikubwa cha kemikali aina ya Zebaki (Mercury) ambazo ni hatari kwa viumbe hai.

Zebaki hiyo hivi sasa imefikia kipimo cha Hg/ug 0.02 kiwango ambacho hakikubaliki kitaifa na kimataifa kwa kuwa kina madhara makubwa kwa viumbe hivyo.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi hizo unaeleza kuwa Zebaki hiyo imefikia hatua ya kuendelea kuingia katika mto Ruvuma hadi katika bahari ya Hindi.


Kwa ujumla mto Lunyere umekuwa ukichafuliwa na wachimbaji wa madini waliopo kwenye eneo la Darpori mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambao huko huchimba madini ya aina mbalimbali hali ambayo inasababisha hata mto Ruvuma na maeneo mengine kuathirika zaidi.

Wataalamu wamekuwa wakisisitiza siku zote kuwa kamwe mtu asiiguse Zebaki kwa kula kupitia chakula au maji kwani ikiguswa inaingia moja kwa moja mwilini kwenye damu na inakwenda kutua kwenye ubongo na kusababisha ubongo kusimama hivyo kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.

Vilevile kemikali hiyo ikisha ingia mwilini mwa binadamu imekuwa ikileta madhara ikiwemo magonjwa kama vile saratani, ulemavu wa akili na hatimaye kifo.


Pia wataalamu wanatahadharisha kuwa ukila samaki wanne tu wenye Zebaki unaweza kuathirika na madhara hayo huchukua miaka mingi kujitokeza ndiyo maana ni vigumu kwa binadamu kutambua kwa haraka kwamba alipata matatizo hayo lini baada ya kutumia bidhaa ambazo zimeathirika na kemikali hiyo.

No comments: