Tuesday, August 29, 2017

WAKURUGENZI WATENDAJI RUVUMA WATAKIWA KUKAMILISHA UJENZI MIRADI YA UMWAGILIAJI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za mkoa huo kukamilisha ujenzi wa skimu zote za umwagiliaji zilizopo mkoani hapa, ili ziweze kuanza kutumika kwa kilimo cha umwagilliaji.

Lengo la kukamilisha ujenzi huo Mkuu huyo wa mkoa alisema utaweza kuleta tija kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao badala ya kutegemea kilimo cha msimu wa mvua.

Dokta Mahenge alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na wakurugenzi watendaji, wenyeviti wa halmashauri na wakuu wa wilaya wa mkoa huo katika kikao cha kazi kilichofanyika Ikulu ndogo mjini Songea.


Alisema kuwa mbali na miradi hiyo kuongeza tija katika uzalishaji itasaidia pia kuongeza thamani ya mazao kwa kuyasindika kabla ya kuuza sokoni.

“Tengeni maeneo maalum pia kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili kuweza kuongeza thamani ya mazao watakayokuwa wanazalisha wakulima, hakikisheni mnaweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa viwanda vya usindikaji vyakula, utengenezaji wa vyakula vya mifugo na mazao mengine”, alisema Dokta Mahenge.

Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuhimiza kuwa kila halmashauri inapaswa kutenga maeneo kwa ajli ya shughuli za viwanda ambavyo baadaye vinapojengwa vinaweza kuleta ajira kwa vijana, wanawake na makundi mengine.


No comments: