Wednesday, August 16, 2017

RC RUVUMA AZIJIA JUU TAASISI ZA UMMA ZISIZOLIPA BILI ZA MAJI SONGEA AAGIZA KUSITISHA HUDUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge akitoa maagizo juu ya kusitisha huduma ya maji kwa idara na taasisi zote za umma zilizopo katika Manispaa ya Songea.
Na Muhidin Amri,       
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Songea (SOUWASA) kusitisha mara moja huduma ya maji kwa idara na taasisi zote za umma zilizopo chini ya Manispaa ya Songea kutokana na deni kubwa la huduma ya maji, lililofikia zaidi ya shilingi milioni 6,574,686.79 ambazo Manispaa hiyo haijaonesha dalili za kulipa deni hilo.

Akizungumza juzi katika kikao maalumu kati  ya viongozi wa SOUWASA na uongozi wa Manispaa hiyo uliowakilishwa na Mhandisi wa maji, Samwel Sanya Dokta Mahenge alisema kuwa amelazimika kutoa agizo hilo  baada ya kuchoshwa na tabia ya viongozi wake kutoonesha ushirikiano licha ya kupewa taarifa ya kuwataka kulipa fedha kwa mamlaka hiyo.

Dokta Mahenge alisema kuwa amechoshwa na tabia ya uongozi wa Manispaa ya Songea chini ya Mkurugenzi wake Tina Sekambo, ambaye mara kwa mara ameonekana kukaidi na kudharau hata maagizo ya viongozi wake wa juu ikiwemo juu ya kulipa madeni ya Wenyeviti wa mitaa ambao wamekuwa msaada mkubwa katika shughuli za kukusanya mapato na ulinzi katika mitaa yao.


“Ninyi Manispaa ya Songea mnatia aibu sana, naagiza kuanzia leo natoa siku saba kwa Mamlaka hii ya maji kuwakatia huduma ya maji katika taasisi zenu zote kama hamtalipa deni mnalodaiwa, mbona umeme mnalipa na hamtaki kulipia huduma ya maji ambayo kwenu ni muhimu”, alihoji Dokta Mahenge.

Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Mahenge alikwenda mbali zaidi na kusisitiza kuwa licha ya Manispaa hiyo kuwa na vyanzo vingi vinavyoiingizia  mapato, lakini  ndiyo inayoongoza kwa madeni na kuwaagiza kulipa madeni yote wanayodaiwa na watu mbalimbali.

Alisema kuwa inasikitisha kuona kila kukicha Manispaa imekuwa ikilalamikiwa na watoa huduma, hata hivyo Mkurugenzi wake amekuwa akionyesha dharau ya maagizo kutoka kwa viongozi na manispaa imeonekana imezoea kudaiwa madeni na watu pamoja na taasisi nyingine za serikali zinazotoa huduma.


Vilevile ameitaka Mamlaka hiyo ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Songea kuchukua hatua kwa wadaiwa wote sugu na kutowaonea huruma kwani endapo wakiendekeza huruma hawataweza kupata fedha wanazodai jambo ambalo litarudisha nyuma juhudi na mikakati yao ya kuongeza mapato na kuboresha huduma zake kwa wananchi.

No comments: