Friday, August 11, 2017

SONGEA YAKABILIWA NA TISHIO LA KUGEUKA KUWA JANGWA

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

WILAYA ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa na tishio la kugeuka kuwa jangwa kutokana na wananchi wanaoishi wilayani humo kukata miti hovyo huku wengine wakichoma misitu moto na baadhi ya watumishi wa serikali wasiokuwa waadilifu kuruhusu wafugaji kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kuingiza idadi kubwa ya mifugo bila kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

Mkuu wa wilaya hiyo, Pololet Mgema alisema hayo jana wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la Madiwani halmashauri wilaya ya Songea kilichofanyika katika kijiji cha Lundusi kata ya Maposeni wilayani humo.

“Kuna uharibifu mkubwa katika mlima Lihanje na nimekuwa nikitoa maagizo kwa watendaji wetu mara kwa mara kusitisha shughuli za kilimo katika mlima ule hata hivyo bado imeonekana baadhi ya wananchi wanaendelea kukata miti hovyo na kuendesha shughuli zao za kibinadamu, kuna watumishi pia ambao ni wagumu kutekeleza maagizo ya serikali sasa mimi mwenyewe nitaanza operesheni ya kuwaondoa ndugu zenu lakini msije kunilaumu kwa hatua nitakayochukua”, alisisitiza Mgema.


Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa ataanza kupita kila kijiji hadi kijiji kwa ajili ya kuwatangazia wananchi kuhusiana na mpango wa serikali kuutunza mlima huo kutokana na umuhimu wake baada ya kuona watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia suala zima la uhifadhi wa mazingira katika mlima Lihanje kushindwa kutimiza wajibu wao kwa sababu wanazozijua.

Mgema amewataka watumishi na madiwani kusimamia ipasavyo agizo la serikali la kutoruhusu uingizaji mifugo kutoka mikoa mingine na kuzuia biashara ya kuchoma mkaa ambayo ndiyo chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu.

Hata hivyo alisema hatua isipochukuliwa mapema kuna hatari kubwa siku za usoni katika wilaya hiyo kuwepo kwa idadi kubwa ya mifugo isiyolingana na ukubwa wa ardhi iliyopo hivyo kuwa na uwezekano wa kutokea vurugu kati ya wakulima na wafugaji wakigombania ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

No comments: