Sunday, August 20, 2017

HALMASHAURI ZAAGIZWA KUKAMILISHA MPANGO WA TAIFA WA VIPIMO KATIKA ZAHANATI NA VITUO VYA AFYA

Na Mwandishi wetu,
Arusha.

SERIKALI hapa nchini, imeagiza Halmashauri zote ambazo hazijakamilisha mpango wa taifa wa kutoa huduma za vipimo kwenye zahanati na vituo vya afya kuhakikisha kwamba inakamilisha huduma hiyo, ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.

Agizo hilo limetolewa juzi na Naibu Waziri wa afya, Dokta Khamis Kigwangala katika ziara yake ya siku tano, wakati alipokuwa akitembelea vituo vya Afya na zahanati za Jiji la Arusha kwa lengo la kuangalia utendaji kazi na changamoto zilizopo katika kutekeleza agizo la uboreshaji wa huduma ya upimaji wa magonjwa mbalimbali.

Dokta Kigwangala alisema kuwa Rais Dokta John Pombe Magufuli alikwisha toa maelekezo ya kuimarisha na kuboresha kwa huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati na vituo hivyo vya afya alipokuwa akifungua kikao cha Bunge mjini Dodoma, kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi ili waweze kupata vipimo vya magonjwa katika maeneo wanayoishi kwa urahisi.

Alisema kuwa Wizara ya afya katika kuhakikisha agizo hilo la Rais Dokta Magufuli linatekelezwa ipasavyo imetoa msisitizo wa utekelezaji huo ikiwemo pia hata sera ya Wizara hiyo inazitaka halmashauri zote kuhakikisha kwamba huduma hiyo ya vipimo vya magonjwa ya kawaida inapatikana kuanzia kwenye ngazi ya zahanati hadi vituo vya afya.


Alifafanua kuwa serikali iliagiza pia kuanzishwa kwa huduma ya upasuaji mdogo na vipimo hivyo lakini inashangazwa kuona halmashauri ya Jiji la Arusha haijatekeleza kikamilifu maagizo hayo.

Vilevile aliongeza kuwa Wizara ya afya ilikwisha toa agizo kwa kusisitiza utekelezaji wake kwenye kikao kilichofanyika Mwandoya wilaya ya Meatu mkoani Simiyu na kwamba haitaki kusikia kwamba kumekuwa na visingizio vinavyokwamisha utekelezaji huo.

Pia alisisitiza kuwa Wizara ipo tayari kuzichukulia hatua  halmashauri zote ambazo zitapuuza maagizo yake kwa kutofanyia utekelezaji kuanzia sasa na hakuna atakayebakia salama iwapo ameshindwa kutekeleza majukumu yake.

Waziri Dokta Kigwangala, licha ya kutembelea maeneo hayo ya vituo vya kutolea huduma ya afya pia amekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo vituo vya afya kutokuwa na vyumba vya upasuaji kwa ajili ya akina mama wajawazito kujifungulia na baadhi ya mashine za kuchunguza magonjwa kutofanya kazi.

Hata hivyo aliagiza kwa kuitaka halmashauri hiyo ambayo inakusanya kodi zaidi ya shilingi bilioni 12 kwa mwaka kutatua kero hizo haraka na kwamba kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Arusha, Rebeca Mongi alisema kuwa halmashauri yake itatekeleza na kutatua kero hizo mapema ikiwemo kukamilisha maelekezo na maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wa afya Dokta Kigwangala.
 


No comments: