Sunday, August 27, 2017

HALMASHAURI ZA WILAYA MKOANI RUVUMA ZATAKIWA KUBORESHA MFUMO WA MANUNUZI


Baadhi ya washiriki wakiwa katika kikao cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

IMEELEZWA kuwa Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani Ruvuma zisipoweka udhibiti wa kutosha katika eneo la manunuzi zitaendelea kuisababishia hasara serikali, hivyo zimetakiwa kuboresha udhibiti huo hasa kwenye kipengele cha manunuzi ya umma na kuweza kuimarisha ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi.

Aidha kila Mkurugenzi katika halmashauri hizo ameagizwa kuwawezesha na kuwatumia wakaguzi wa ndani kikamilifu katika kutathimini ufanisi wa mifumo ya udhibiti wa ndani na kuchukua hatua stahiki, sambamba na kuziwezesha kamati za ukaguzi katika kutekeleza majukumu yao.

Mkuu wa mkoa huo, Dokta Binilith Mahenge alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2015/2016 kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Ikulu ndogo mjini hapa.


“Katika eneo hili nataka kila halmashauri iendelee kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi watakaobainika kuhusika na vitendo vya ubadhirifu au kutowajibika ipasavyo na kuisababishia hasara serikali”, alisema Dokta Mahenge.

Dokta Mahenge aliongeza kuwa kufanyika kwa kikao hicho ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambayo yanawataka Wakurugenzi wote katika halmashauri kuhakikisha kwamba hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinajadiliwa na hatua za kisheria na nidhamu zinachukuliwa kwa wakati dhidi ya wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki kuwepo kwa hujuma mbalimbali.

Pia alisisitiza kuwa ni wajibu kwa kila Mkurugenzi kwa kushirikiana na Madiwani wahakikishe mifumo ya hoja za miaka ya nyuma kwa kila mwaka wa fedha zinajibiwa ipasavyo na kufungwa kwa wakati.

Naye Mwakilishi wa CAG mkoani Ruvuma, Suleiman Mwaliwale akizungumza katika kikao hicho alieleza kuwa wameweza kubaini mapungufu mbalimbali ndani ya halmashauri ikiwemo kutokuwa na mifumo mizuri ya ndani ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, michakato ya uteuzi wa wakandarasi kutofuata taratibu husika na kusababisha miradi ya maendeleleo ya wananchi kutekelezwa chini ya kiwango.

Alisema kumekuwa pia na udhaifu wa ukaguzi wa vitengo vya ndani ambapo hali hiyo inasababishwa na uhaba wa rasilimali watu na kutengewa fedha bajeti ndogo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pamoja na mambo mengine, wakichangia hoja kwa nyakati tofauti wajumbe waliohudhuria kikao hicho walimweleza Mkuu wa mkoa huo Dokta Mahenge kwamba watatekeleza maagizo ya serikali ipasavyo na kurekebisha kasoro zilizopo ili zisiweze kujirudia tena katika mwaka wa fedha ujao.


Hata hivyo kikao hicho cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hapa mkoani Ruvuma kilihusisha viongozi wake wa kutoka ndani ya halmashauri za mkoa huo ambazo ni wilaya ya Songea, Mbinga, Namtumbo, Tunduru na Manispaa ya Songea.

No comments: