Monday, August 21, 2017

NYASA WANUFAIKA NA WASAIDIZI WA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU

Ziwa Nyasa.
Na Julius Konala,   
Nyasa.

MKUU wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Isabella Chilumba amelipongeza shirika lisilo la kiserikali la Wasaidizi wa Sheria na Haki za Binadamu (WASHEHABINYA) wilayani humo kwa kuendesha mafunzo juu ya utawala bora kwa wananchi pamoja na viongozi wa vijiji na kata, ambayo yameweza kuwajengea uwezo namna ya kuishi na kufanya shughuli zao za kimaendeleo.

Aidha mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tatu katika kata nne za wilaya hiyo ambayo yamefadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil Society (FCS) kutoka Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa wilaya hiyo, Chilumba ndiye aliyefungua mafunzo hayo juzi mjini hapa yaliyoshirikisha baadhi ya wananchi, wenyeviti wa vitongoji, vijiji, pamoja na maofisa watendaji wa kata.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mradi huo umefika wakati muafaka kwa kile alichoeleza kuwa wananchi wengi hawajui haki zao za msingi, kutokana na kutojua sheria pamoja na kushindwa kesi zao mbalimbali Mahakamani kwa sababu ya ukosefu wa msaada wa kisheria.


Chilumba alisema kuwa kutokana na baadhi ya wananchi  na watendaji wilayani  humo kutojua sheria wamekuwa wakikiuka taratibu mbalimbali ikiwemo kufanya uchafuzi wa mazingira, kwa kuosha magari na pikipiki zao ufukweni mwa ziwa Nyasa hali ambayo inasababisha mafuta ya vyombo hivyo vya moto kuchanganyika na maji na kupelekea upatikanaji wa samaki  ndani ya ziwa hilo kuwa mgumu.

Katika kukabiliana na tatizo hilo Mkuu huyo wa wilaya amewataka pia washiriki  wa mafunzo hayo kuzingatia na kufuatilia kwa umakini mada walizofundishwa na wakufunzi hao ili waweze kuboresha utendaji kazi wao pamoja na kuwajengea uwezo wa jinsi ya ufuatiliaji wa rasilimali za taifa.

Awali Mratibu wa shirika hilo, Jacob Ngonyani akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Chilumba alieleza kuwa Wasaidizi hao wa sheria na haki za binadamu ni asasi ambayo ipo katika mchakato wa kutekeleza sera ya taifa ya maendeleo hivyo wametekeleza mradi huo katika kata nne za wilaya hiyo.

Ngonyani alizitaja kata zitakazonufaika na mradi huo kuwa ni kata ya Kilosa, Mbamba bay, Lipingo pamoja na kata ya Liuli ambapo amedai kuwa dhumuni la shirika hilo ni kutoa elimu ya sheria na haki za binadamu, kutoa msaada wa kisheria kwa jamii, jinsi ya ufuatiliaji wa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, kutoa ushauri na kusimamia haki za waathirika waishio na Virusi Vya Ukimwi (VVU), kushirikiana na taasisi nyingine ndani na nje ya nchi na kufanya utafiti.

Aliongeza kuwa pia hutoa elimu juu ya masuala ya usawa wa kijinsia, afya ya jamii, utawala bora, umaskini wa kipato, mazingira, kilimo, utamaduni, vijana wanawake na watoto huku akidai kuwa dhamira ya shirika hilo ni kuhakikisha jamii inajengewa pia uwezo katika masuala ya sheria na haki za binadamu.

Naye mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo Mnung’a Mnung’a alisema kuwa ili Tanzania iweze kufikia malengo iliyojiwekea ni lazima kazi na nguvu za pamoja zitumike katika kujenga uchumi pamoja na ushirikishwaji wa sekta mbalimbali.

Mnung’a alifafanua kuwa sababu kubwa iliyosababisha kuchelewa kufikiwa kwa dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 ni ukosefu wa usimamizi wa rasilimali mbalimbali za taifa, wananchi kutowajibika pamoja na kukithiri kwa ubadhirifu serikalini jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ndani ya nchi.

Aidha mwezeshaji mwingine, Wilgis Komba alibainisha kuwa ili Tanzania iweze kufikia dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 watumishi wa umma wanatakiwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uaminifu, kuepuka ubinafsi, uwajibikaji, uwazi, kuheshimu sheria pamoja na kuacha vitendo vya upendeleo.

Komba aliwataka viongozi kutumia hekima na busara pindi wanapotimiza majukumu yao, kuzingatia utii wa sheria, watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma pamoja na wananchi kuwajibika ipasavyo badala ya kutegemea kila kitu wafanyiwe na serikali.


Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Vailet Nkondola alilipongeza shirika hilo la WASHEHABINYA kwa kuwajengea uwezo wa masuala ya utawala bora huku akiliomba waendelee kuongeza wigo wa mradi huo, ili uweze kuwafikia wananchi wengi waishio vijijini ambao bado hawajui namna ya kupata haki zao za msingi.

No comments: