Wednesday, August 9, 2017

TASAF SONGEA YAANZA NA MFUMO WA MALIPO KWA NJIA YA MTANDAO KAYA MASKINI


Wataalamu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakiwa pamoja na wanufaika wa mfuko huo wakati wakikagua manufaa ya matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao.
Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, umeanza kutoa malipo kwa njia ya mtandao kwa kaya maskini 4,959 zilizopo katika mpango wa kunusuru kaya hizo katika Manispaa hiyo.

Christopher Ngonyani ambaye ni Mratibu wa TASAF katika Manispaa ya Songea alisema kuwa wanufaika 604 tayari wamesajiliwa kwa ajili ya kulipwa kwa njia ya mitandao ya simu, ambapo kati yao wanufaika 475 wameingiziwa fedha zao katika malipo ya mwezi Julai hadi Agosti mwaka huu.

Alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba wanufaika wote wanaingizwa kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao ambapo malipo yatakuwa yanalipwa moja kwa moja na TASAF kutoka makao makuu ya mfuko huo badala ya fedha za wanufaika hao kutumwa kupitia halmashauri husika kama ilivyokuwa hapo awali.


“Jumla ya shilingi milioni 16.5 zimelipwa wiki hii kwa kaya maskini 475 moja kwa moja kutoka makao makuu ya ofisi za mfuko huu, na hivi sasa tayari kaya hizi zimepata fedha zao kwa njia ya mitandao ya simu zao na wale ambao hawajasajiriwa bado hawajalipwa”, alisema Ngonyani.

Ngonyani alieleza kuwa kaya 4,484 ambazo bado hazijasajiriwa kwenye mfumo huo wa malipo kwa njia ya simu zitalipwa fedha zao kwa njia ya fedha taslimu kuanzia wiki ijayo ambapo ni zaidi ya shilingi milioni 155.9.

Alisisitiza kuwa mpango uliopo ni kuhakikisha kwamba wanufaika wote wa TASAF wanajisajiri kulipwa kwa njia ya mtandao wa simu ili kuepukana na changamoto zilizopo ambazo hujitokeza katika malipo ya fedha taslimu ikiwemo kuepukana na malipo hewa.

Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii katika Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na watendaji waliopo makao makuu ya ofisi za mfuko huo kitengo cha malipo kwa njia ya mtandao, wamekuwa wakitembelea katika mitaa ya wanufaika husika katika Manispaa hiyo ili kuangalia changamoto zilizopo kwenye mfumo mpya wa malipo kwa njia hiyo ya mtandao huku wakihamasisha wanufaika wengine waendelee kusajiri.

Utafiti uliofanywa katika mitaa mbalimbali iliyopo katika Manispaa hiyo ambayo wanufaika hao wamelipwa fedha kwa njia ya mtandao, imebainika kuwa mfumo huo umepata mafanikio makubwa baada ya wanufaika wengi kupata fedha zao bila kujitokeza matatizo yoyote yale jambo ambalo wanufaika wasiojisajiri kuhamasika kuingia kwenye mfumo huo.

Manispaa ya Songea ni moja kati ya halmashauri 16 hapa nchini zilizochaguliwa kufanya majaribio ya malipo kwa njia ya mtandao wa simu kwa wanufaika wa TASAF ili kuepukana na changamoto zilizokuwa zimejitokeza kupitia mfumo wa kulipwa fedha taslimu.

Pamoja na mambo mengine, mpango wa kunusuru kaya maskini umekuwa ukiendeshwa katika halmashauri 163 hapa nchini na kwamba mpango huu umeweza kuzinufaisha kaya maskini ikiwemo zile ambazo hapo awali zilikuwa zikipata mlo mmoja kwa siku ambapo hivi sasa zinapata milo mitatu kwa siku.

No comments: