Monday, August 21, 2017

WADAU WAPINGA ENEO LA UJENZI OFISI ZA HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga

BAADHI ya Wadau wa maendeleo na mazingira katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameanza kupinga hoja iliyopitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo, juu ya ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo ambazo zinatarajiwa kujengwa katika eneo maarufu linalofahamika kwa jina la Ndengu lililopo katika kata ya Nyoni wilayani hapa.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye.

Wadau hao walisema hayo kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wakidai kwamba hawakubaliani na maamuzi hayo kwani eneo hilo ambalo wanataka kujenga ofisi hizo, lilitengwa na kuhifadhiwa kwa miaka mingi kwa ajili ya kutunza mazingira na vyanzo vya maji vilivyopo huko ambavyo ndiyo tegemeo kubwa kwa ajili ya kulisha wakazi wa mji wa Mbinga.

Aidha walifafanua kuwa wakiwa kama wadau wakubwa wa mazingira wanatambua kuwa pale panapojitokeza kuwa na uwekezaji mkubwa kama huo ni lazima kwanza kufanyike tathimini ya athari za mazingira katika eneo kama hilo ambako ujenzi wa ofisi hizo wanataka kuufanya kwa kushirikisha maoni ya wataalamu wa sekta ya mazingira na sio kuchukua maamuzi kama hayo peke yao.

“Unajua leo panapokuwa na makazi katika eneo kama lile ni lazima uzalishaji wa taka utakuwa mkubwa hasa kipindi cha masika mvua zitakapokuwa zinanyesha maji yake yatakayokuwa yanatiririka ambayo yamebeba taka nyingi zitakazokuwa zinazalishwa pale, zitakuwa zinaangukia kwenye bonde lile ambalo lina vyanzo vya maji vinavyolisha wakazi wa mji huu ni lazima jambo hili tunapaswa kuwa waangalifu”, alisema Jordan Ndunguru.


Vilevile Ndunguru aliongeza kuwa kuna kila sababu sasa kwa serikali kuangalia upya jambo hilo na kuchukua hatua mapema ya kulizuia kabla mazingira hayo hayajaharibiwa ili kuweza kuyanusuru kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Naye Joackimu Komba aliongeza kuwa miaka mitatu iliyopita serikali ilihamisha mashamba ya kahawa na makazi ya watu waliokuwa wakiishi katika eneo hilo la Ndengu, lakini leo wanashangazwa na kitendo cha Madiwani hao kukubaliana katika vikao vyao kwamba wanataka kujenga majengo ya ofisi za halmashauri ya wilaya huku wakijua fika kwamba eneo hilo ndilo ambalo linavyanzo vikuu vya maji ambavyo ni tegemeo kubwa kwa kulisha watu wanaoishi mjini hapa.

Pia alisema kuwa shughuli za kibinadamu ambazo zitakuwa zinaendelea kufanyika katika eneo hilo zitakuwa zina athari kubwa zikiathiri vyanzo vya maji ambapo maamuzi hayo yanakinzana kabisa na sheria ya mazingira juu ya sura ya uboreshaji wa vyanzo hivyo ambapo ni vyema sasa sheria ya athari ya mazingira ya mwaka 2004 ikazingatiwa na kuheshimiwa, pafanyike tathimini kwanza kabla ya Wizara husika kupitisha hoja hiyo ya Madiwani hao juu ya ujenzi wa makao makuu ya ofisi zao za wilaya.

“Kuna maeneo mengine mengi ndani ya wilaya ya Mbinga ambayo yanafaa pia kwa ujenzi wa miundombinu ya majengo haya ya wilaya hii, kwa nini wang’ang’anie pale kwenye vyanzo vya maji ambavyo ndiyo tunapata maji safi na salama yanayotufanya tuendeshe uhai wa maisha yetu”, alisema Komba.

Pamoja na mambo mengine, maamuzi hayo ya ujenzi wa ofisi za wilaya hiyo yalifikiwa Agosti 17 mwaka huu katika kikao cha Baraza la Madiwani hao kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa, baada ya uwepo wa mvutano mkubwa uliodumu kwa masaa kadhaa kati ya Madiwani hao na Watendaji wa halmashauri hiyo juu ya wapi ofisi hizo zitajengwa.

Awali zilipopigwa kura kwa lengo la kukubaliana kwamba ujenzi huo ukafanyike katika eneo la Kiamili lililopo katika kata ya Kigonsera, Madiwani hao walikataa na kukubaliana kwamba zipigwe kura kwa mara ya pili kwa kuchagua kati ya eneo la Maguu, Ndengu na Matiri.

Zilipopigwa kura kwa awamu nyingine ya pili kuchagua maeneo hayo ndipo eneo la Ndengu lilishinda kwa kura 24, likifuatiwa na Matiri kwa kura 9 na Maguu kwa kura 1 huku kura mbili zikiharibika kati ya wapiga kura 36 waliokuwepo katika kikao hicho.


Kwa ujumla halmashauri ya wilaya ya Mbinga imefikia hatua ya kuhama katika ofisi zake za awali zilizopo mjini hapa na kwenda kujenga miundombinu mingine mipya ya wilaya hiyo katika eneo lingine, baada ya kugawika na kuizaa halmashauri nyingine ya mji wa Mbinga ambayo ndiyo inapaswa kutumia majengo hayo yaliyopo sasa mjini hapa.

No comments: