Thursday, August 3, 2017

VIUA WADUDU KUTOKOMEZA MALARIA SONGEA MKOANI RUVUMA

Afisa afya wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Dokta Vitalis Mkomela hivi karibuni akikabidhiwa sehemu ya lita 1,000 za Viuawadudu toka kwa Waziri wa afya Dokta Ummy Mwalimu.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

SERIKALI hapa nchini imeongeza chachu katika mapambano dhidi ya ugonjwa Malaria, baada ya kununua lita laki moja za dawa ya kuua mbu na kusambazwa maeneo mbalimbali ili kuweza kukabiliana na mazalia ya wadudu wanaoeneza ugonjwa huo.

Viuadudu vya kutokomeza mbu wa malaria vinatengenezwa katika kiwanda cha kuzalisha Viuadudu kilichopo mjini Kibaha mkoani Pwani, ambapo halmashauri 14 nchini ikiwemo ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma zina viwango vikubwa vya maambukizi ya ugonjwa wa malaria.

Kufuatia hali hiyo tayari Manispaa hiyo imepokea dawa hiyo na hivi sasa yanafanyika maandalizi ya kuanza kupulizia makazi ya wananchi ili kuweza kutokomeza ugonjwa huo.

Afisa afya na mazingira wa Manispaa ya Songea Dokta Vitalis Mkomela alisema kuwa wamepokea lita 1,000 za dawa hiyo, ambazo zimenunuliwa na Rais Dokta John Magufuli ambapo kiasi hicho cha dawa kinatosha kupulizia katika kipindi hiki cha kiangazi katika mitaa 95 ya Manispaa hiyo.


Dokta Mkomela alisema kuwa kabla ya kuanza kazi ya kupulizia yanaandaliwa mafunzo na miongozo kwa wafanyakazi wa kujitolea 95, wenyeviti wa mitaa 95 na maafisa afya ambao watapewa elimu ili waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

“Idara itanunua pampu 98 zitakazotumika katika zoezi hili, pia unahitajika usafiri ili wafanyakazi waweze kuanza kazi mapema kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa tano asubuhi”, alisema.

Vilevile alieleza kuwa mazalia ya mbu yakipungua, mbu wa malaria pia watapungua na hatimaye ugonjwa huo utaweza kufikia hatua ya kutokomezwa katika Manispaa hiyo.

Ili kuhakikisha zoezi hilo linatoa matokeo makubwa Dokta Mkomela alisisitiza kuwa kila dimbwi la maji lenye mazalia ya mbu litapuliziwa mara nne kwa mwezi sawa na kupulizia mfululizo kila baada ya siku saba na kwamba watapulizia pia mazalia ya mbu yaliyofunikwa na yale yaliyokuwa wazi.

Aliongeza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu ambapo katika kipindi cha masika Manispaa itanunua dawa za kupulizia mazalia yote ambayo yatakuwepo katika kipindi hicho ili kuhakikisha kuwa mazalia ya mbu yanatokomezwa kabisa.


Hata hivyo jumla ya watu 133 katika halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani hapa wamefariki dunia mwaka 2015 baada ya kuugua ugonjwa wa malaria huku Watanzania 60,000 nao wanakufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo ambapo pia kila siku hapa nchini watu 291 wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na malaria.

No comments: