Baraza la Madiwani Halmashauri Mji wa Mbinga, likiwa limeketi juzi kwenye kikao chake cha robo ya pili katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo mjini hapa. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri
ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma limemfukuza kazi aliyekuwa Kaimu Afisa misitu wa
Halmashauri hiyo, David Hyera kwa kile walichoeleza kuwa baada ya kupatikana na
hatia ya kutosimamia na kutekeleza majukumu yake ya kazi za utumishi wa umma
ipasavyo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza
hilo cha robo ya pili kilichoketi juzi mjini hapa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kipwele
Ndunguru alisema kuwa hatua ya kumfukuza kazi mtumishi huyo pia inatokana na
kushindwa kusimamia mapato ya fedha za mradi wa uvunaji wa msitu.
Ndunguru aliutaja msitu huo kuwa ni
wa Mbambi ambao ni wa Halmashauri ya Mji huo na kwamba baada ya Hyera kushindwa
kutekeleza kikamilifu majukumu aliyopewa alisababisha kutokea kwa wizi wa mbao na
upotevu wa mamilioni ya fedha za mradi huo.
“Kamati ilipochunguza makosa yake
ilimkuta ana hatia na kamati ilipendekeza apewe adhabu ya kufukuzwa kazi”,
alisema Ndunguru.
Awali Baraza hilo lilisema kuwa
kufuatia uzembe huo uliofanywa katika mradi huo wa uvunaji msitu wa Mbambi, wamepata
hasara zaidi ya shilingi milioni 800.
Hata hivyo maamuzi hayo ya Baraza
hilo yalifikiwa baada ya Kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga,
Cosmas Nshenye kutoa taarifa yake ya uchunguzi katika baraza la dharula
lililoketi Novemba 20 mwaka jana kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo
mjini hapa, ambapo baada ya kufanya uchunguzi huo waliweza kubaini mapungufu
yaliyojitokeza katika shughuli hiyo ya uvunaji wa msitu.
No comments:
Post a Comment