Monday, January 1, 2018

SERIKALI KUENDELEA KUTOA KIBANO KWA VIONGOZI WA UMMA



Na Mwandishi wetu,

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi zote za maadili zilizopo hapa nchini, zimeagizwa kuhakikisha kwamba viongozi hawafanyi biashara na Ofisi za umma.

George Mkuchika.
Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa nchi, ofisi ya Rais, (Utumishi na utawala bora, George Mkuchika wakati alipokuwa akikabidhi fomu ya tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa utumishi wa umma katika ofisi za maadili Kanda ya kusini mkoani hapa.

Alisema Wizara yake imekuwa ikipokea taarifa kwamba wapo madiwani, wabunge na wakuu wa mashirika ya umma hufanya biashara na halmashauri zao, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.


Sheria ya maadili imekuwa ikizungumzia suala la mgongano wa maslahi ambapo viongozi kumiliki kampuni ambayo imeandikishwa kwa jina la mtu mwingine au kuwa na kampuni ambayo wana hisa ni kinyume cha sheria.

Kadhalika, sheria inawazuia viongozi hao kukaa kwenye vikao na kuamua mtu wa kupewa zabuni kwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma.

“Wewe mheshimiwa diwani kuwa na kampuni yako ambayo umeandikisha jina la mtu mwingine au kuwa na kampuni yako ambayo wewe una hisa, lakini wakati huo huo unakaa kwenye kikao na kuamua nani apewe tenda katika halmashauri yako hilo ni kosa kwa mujibu wa maadili”, alisema Mkuchika.

Vilevile Mkuchika alielezwa kuwa Ofisi hiyo inakabliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji ikiwamo vitendea kazi na rasilimali fedha, hali ambayo inasababisha kushindwa kuwafikia viongozi wa umma na ambapo aliombwa aone namna ya kuweza kutatua changamoto hiyo.

Naye Katibu msaidizi katika ofisi hiyo, Mayina Henjewele alisema kuwa changamoto hizo zimekuwa zikikwamisha kwa kiasi kikubwa utendaji wa kazi zao.

Pamoja na mambo mengine Waziri Mkuchika aliwaahidi na kuwahakikishia kwamba changamoto wanazokabiliana nazo watumishi hao atazifanyia kazi.

No comments: