Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
AGIZO la Serikali la kutaka kujengwa
na kukarabatiwa kwa vituo 172 vya afya kote nchini na kuhakikisha kwamba kazi hiyo
iwe imekamilika ifikapo Desemba 30 mwaka huu, hali hiyo imekuwa kinyume kwa
Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma ambapo mpaka sasa ujenzi wa Kituo
cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu ndani ya halmashauri hiyo
haujakamilika.
Hilo limebainika kufuatia malalamiko
yaliyotolewa na Diwani wa kata hiyo, Dustan Ndunguru na wananchi wake wakieleza
kuwa licha ya kituo hicho kupewa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 lakini
hali ya maendeleo ya ujenzi wake imekuwa ikifanyika kwa kusuasua.
Diwani huyo na wananchi wake wamemlalamikia
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Robert Kadaso Mageni wakimtuhumu kwamba
ndiye aliyesababisha na kukwamisha kutokamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kwa
wakati uliopangwa kulingana na agizo lilitolewa na Serikali.
Ndunguru alisema kuwa Serikali licha
ya kuwataka viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kuhakikisha wanasimamia kazi
hiyo iwe imekamilika ifikapo Desemba 30 mwaka jana na baada ya hapo, iweze
kuweka vifaa tiba vya kuweza kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya
hali hiyo imekuwa kinyume hivyo aliongeza kuwa kuna kila sababu ya mamlaka
husika ngazi ya juu Serikalini kuchukua hatua ili iweze kuwa fundisho kwa
viongozi wengine ambao ni wazembe katika kusimamia miradi ya maendeleo ya
wananchi.
Alisema kuwa tokea ujenzi huo uanze
kufanyika katika kata yake ya Kihungu kumekuwa na uzembe mkubwa ukifanyika wa
uagizaji wa vifaa vya ujenzi na malipo kwa mafundi waliokuwa wakifanya kazi ya
ujenzi jambo ambalo lilisababisha hata baadhi yao kugoma kuendelea kufanya
kazi.
“Pamoja na Serikali kutaka hata
malighafi zinazopaswa kutumika katika shughuli ya ujenzi zitumike zile ambazo
zinapatikana karibu na eneo la ujenzi unapofanyika kama vile mchanga, hapa
kwangu tokea ujenzi huu uanze kutekelezwa mchanga umekuwa ukichukuliwa mbali katika
maeneo ya kata ya Mkako na Maguu licha ya hapa katika kata hii kupatikana mchanga
mwingi unaofaa kufanyia kazi hii”, alisema Ndunguru.
Pia alisema kuwa anashangazwa na hata
hivi sasa kituo hicho cha afya hakina msimamizi yaani wataalamu wa ujenzi ambao
wangeweza kushauri na kusimamia shughuli za ujenzi zinazoendelea hapo badala
yake wameachwa mafundi peke yao wakifanya kazi bila usimamizi wa karibu.
Aliongeza kuwa Mkurugenzi huyo wa mji
wa Mbinga, Mageni ndiye aliyewafukuza wataalamu ambao ni Wahandisi wasaidizi
waliokuwa hapo awali wakisimamia ujenzi huo na kwamba kuwafukuza huko alidai
kuwa kunatokana na maslahi yake binafsi aliyonayo ya kutaka aweze kupata mwanya
wa kufanya ubadhirifu wa fedha za mradi huo.
“Hata bati za kuezekea majengo ya
kituo hiki cha afya zimekuwa pungufu baadhi ya majengo hayajaezekwa, usakafiaji
wa majengo haujafanyika vifaa vya ujenzi kama vile saruji vimekuwa vikiletwa
hapa kwa kusuasua ndiyo maana hata spidi ya ujenzi hakuna”, alisema.
Nao baadhi ya wananchi wa kata ya Kihungu
wakizungumza kwa nyakati tofauti walidai kuwa kukwama kwa mradi huo
kutokamilika kwa wakati ni kiburi alichonacho Mkurugenzi huyo ambacho
kinadhihirisha wazi kuwa hata aliyekuwa Naibu Waziri wa afya, maendeleo ya
jamii, jinsia, wazee na watoto Dokta Khamis Kigwangala aliyetembelea kituo
hicho mapema Julai 15 mwaka jana na kumtaka Mkurugenzi huyo kutekeleza agizo la
ukarabati wa majengo yaliyopo hapo awali ya kituo cha afya Kalembo, ujenzi wa
jengo la maabara na upasuaji katika eneo hilo la kituo lakini mpaka leo hii
hakuna kilichofanyika licha ya Waziri huyo kutoa miezi mitatu kazi hiyo iwe
imekamilika.
Walidai kuwa Serikali kuendelea
kumfumbia macho mtumishi kama huyu ambaye hatekelezi kwa wakati maagizo na
maelekezo yanayotolewa na viongozi wake wa ngazi ya juu ni sawa na kurudisha
nyuma maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Mageni alipohojiwa juu ya hali hiyo alikataa
kutolea ufafanuzi tuhuma hizo huku akimjibu jeuri mwandishi wetu licha ya mwandishi huyo kwenda Ofisini kwake kutaka ufafanuzi zaidi.
Hata hivyo Serikali kwa ujumla ilitoa
fedha zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya
Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu halmashauri ya mji wa Mbinga kwa ajili
ya kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi wa jengo la upasuaji, maabara, wodi ya
akina mama na watoto, nyumba ya mganga pamoja na jengo la kuhifadhia maiti
ambapo mpaka sasa ujenzi wake bado haujakamilika.
No comments:
Post a Comment