Na Muhidin Amri,
Songea.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka Watanzania kutembea kifua mbele wakati huu ambao Serikali ya awamu ya tano inaendelea kumaliza kero, kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuimarisha uchumi.
Majaliwa alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na wakazi wa mtaa wa Unangwa kata ya Seed Farm katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa gridi ya Taifa kutoka Njombe hadi Songea mkoani Ruvuma.
Alisema kuwa Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi huo ambao tayari umeshaanza kutekelezwa katika mkoa wa Njombe na sasa umefika Ruvuma, kwa hiyo wananchi wajiandae kutumia fursa ya umeme wa uhakika ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili kukuza kipato na uchumi wa nchi.
Aliwataka wananchi kuwa na matumaini makubwa na Serikali yao ambayo inataka kuona kila Mtanzania anafikiwa na huduma bora za kijamii ikiwemo nishati ya umeme ambayo itasambazwa hadi vijijini.
“Umeme huu utasaidia sana wakazi wa mkoa huu kujiimarisha kiuchumi, nawaomba wananchi muanze kujiandaa kutumia fursa hii ambayo Serikali imepanga kuhakikisha kwamba kila mmoja anafaidika nayo", alisema Waziri Mkuu.
Aidha amemtaka mkandarasi wa mradi huo kujenga kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilisha kwa wakati uliopangwa ili wananchi waweze kupata huduma ya umeme na kumaliza changamoto zao zinazosababishwa na ukosefu wa umeme wa uhakika.
Pia Waziri Mkuu, Majaliwa ameipongeza Serikali ya Sweden kwa uamuzi wake wa kutoa fedha za mradi huo na miradi mingine hapa nchini na kusisitiza kuwa Tanzania, itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa Serikali.
No comments:
Post a Comment