Na Muhidin Amri,
Madaba.
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO)
Mkoani Ruvuma, limeagizwa kufanya jitihada ya kupeleka nishati hiyo haraka
katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani humo, ili watumishi waliopo huko
waweze kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma bora kwa wananchi ipasavyo.
Aidha imeelezwa kuwa umeme huo
utasaidia kupunguza gharama kubwa ya uendeshaji wa Ofisi kutokana na kutumia
mafuta mengi kwa ajili ya kuendeshea Jenereta pale watumishi hao wanapofanya
kazi husika.
Palolet Mgema ambaye ni Mkuu wa
Wilaya ya Songea alitoa agizo hilo juzi ambapo alisema kuwa anataka kuona TANESCO
wanapeleka umeme haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo isiendelee kuwepo.
Umeme huo alisema kuwa endapo ukifika
huko utaweza kurahisisha hata utendaji kazi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
Mgema alitoa kauli hiyo baada ya baada
ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Shafi
Mpenda kwamba hadi sasa hawana huduma hiyo licha ya umeme kuanza kuwaka tangu mwezi
Desemba mwaka jana.
Mpenda alisema jambo hilo limekuwa
likichangia baadhi ya kazi kukwama ikiwemo hata kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki
(EFDS) kwa ajili ya kukusanyia mapato ya Serikali.
Alisema kuwa TANESCO ndiyo wamekuwa
kikwazo na tatizo kubwa kutokana na kushindwa kupeleka umeme katika Ofisi za
halmashauri hiyo licha ya kutoa taarifa ya kuomba kuunganishiwa nishati hiyo
muda mrefu uliopita.
“Tukipata nishati hii itatusaidia kupunguza
gharama ya matumizi ya mafuta kwa ajili ya kuendesha Jenereta ambalo limekuwa likitugharimu
fedha nyingi pale tunapotaka kutumia vifaa vya umeme”, alisema Mpenda.
No comments:
Post a Comment