Thursday, January 4, 2018

WAZIRI MKUU KUANZA ZIARA YA KIKAZI LEO MKOANI RUVUMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa upande wa kulia akipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme katika uwanja wa ndege Songea akiwa katika siku yake ya kwanza kati ya siku tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Na Muhidin Amri,    
Songea.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameanza ziara yake ya siku tatu kuanzia leo Januari 4 hadi 9 Mkoani Ruvuma, ambapo katika ziara hiyo atatembelea Wilaya ya Songea, Mbinga na Nyasa zilizopo mkoani humo.

Mkuu wa mkoa  huo, Christine Mndeme alisema kuwa katika ziara hiyo Waziri Mkuu ataweka mawe ya msingi na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na ile iliyotekelezwa ndani ya wilaya hizo.

Kwa mujibu wa Mndeme alifafanua kuwa miradi hiyo ni ile ambayo inalenga kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi katika maeneo atakayotembelea.


Aidha alibainisha kuwa akiwa mkoani hapa, Waziri Mkuu atakutana na kuzungumzia na watumishi wa umma kwa lengo la kuwakumbusha majukumu na wajibu wao kwa kila mtumishi katika kuwatumikia wananchi, pamoja na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma amewataka wananchi wa maeneo yote ambayo Waziri Mkuu atatembelea wajitokeze kwa wingi kumpokea wakati wote ambao Waziri atakutana nao.

Alisema kuwa Januari 5 ambayo ni siku ya Ijumaa Waziri Mkuu Majaliwa ataanza ziara yake kwa kukagua mradi wa shamba la kahawa la Kampuni ya Aviv Tanzania Limited, lililopo kijiji cha Lipokela Wilaya ya Songea na baadaye kuwasili Wilayani Mbinga na Nyasa.

No comments: