Na Mwandishi wetu,
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto imesema kwamba kuanzia mwezi Aprili mwaka huu itaanza
kutoa bure chanjo dhidi ya kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi
(Human Papillon Virus) kwa wasichana kuanzia umri wa miaka 14.
Aidha hatua hiyo inatokana na takwimu
za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 kuonyesha kuwa Tanzania
inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wapya wa saratani ya mlango wa kizazi 51
kwa kila wanawake 100,000 huku vifo vikiwa 38 kwa kila wanawake 100,000,
ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dokta
Faustine Ndugulile alisema hayo jana alipokuwa akizindua kampeni ya uchunguzi
wa mabadiliko ya awali ya saratani hiyo na ya matiti, uliofanyika katika
Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.
Alisema hatua hiyo ya chanjo inalenga
kukinga kirusi kinachoeneza saratani ya mlango wa kizazi ambayo Tanzania
inaongoza kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na wagonjwa wengi.
Vilevile alisema kuwa katika awamu ya
kwanza ya utoaji wa chanjo hiyo mwaka huu wamepanga kuwafikia wasichana wa
kuanzia miaka 14 wapatao 616,734.
“Hawa 616,734 ndio tumepanga
kuwapatia chanjo mwaka huu na katika mwaka ujao tutawafikia wasichana wa
kuanzia miaka tisa hadi 14 na mwaka utakaofuata tutawapa chanjo wale wenye umri
wa kuanzia miaka tisa”, alisema Dokta Ndugulile.
Alifafanua kuwa chanjo hiyo itasaidia
kuwalinda wasichana ambao wako katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa virusi
vinavyosababisha saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
"Saratani ya mlango wa kizazi
moja ya sababu ambazo zinachangia ni wasichana kushiriki ngono katika umri
mdogo, kuwa na wenza wengi lakini pia kubeba mimba nyingi kunaweza kusababisha
mtu kupata maambukizi”, alisema.
Aliwataka akinamama kupima afya zao
mara kwa mara na wanapobainika kuwa na maambukizi, wanatakiwa kuwaona wataalamu
ili kupatiwa matibabu.
Alieleza kuwa saratani hii inatibika
kabisa kama mtu atapata vipimo vya afya yake kila mara, lakini watu wengi
wamekuwa wakija katika hospitali wakiwa wamechelewa hali ambayo saratani inakuwa
imesambaa katika maeneo mengine ya mwili kama vile mifupa, ini na damu na kuwa
vigumu kutibika.
Dokta Ndugulile aliwaagiza Wakuu wa
mikoa yote hapa nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia upimaji wa saratani ya
mlango wa kizazi katika mikoa yao ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ilivyojipangia
hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu iwe imefikia akinamama milioni tatu.
Aliongeza kuwa pamoja na juhudi hizo
pia Serikali hivi sasa inaboresha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI)
ambayo ni taasisi pekee nchini katika kukabiliana na tatizo la saratani, kwa
kuweka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia kutoa huduma za matibabu ambazo zilikuwa
zinatolewa nje ya nchi.
Katika mwaka 2016 Taasisi hiyo ilipokea
wanawake 1,934 wa saratani ya mlango wa kizazi huku takwimu hizo zikizidi
kuongezeka na kwamba jamii inapaswa kuhamasika namna ya kupambana na ugonjwa
huo.
No comments:
Post a Comment