Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zinaendelea kujengwa. |
Na Albano Midelo,
Songea.
HATIMAYE Kampuni ya kimataifa ya
China, inayofahamika kwa jina la China Sichuan International Co-operation
imeshinda Zabuni ya kuendelea na ujenzi wa barabara za Manispaa ya Songea Mkoani
Ruvuma kwa kiwango cha lami nzito.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Tina
Sekambo alisema kuwa Kampuni hiyo inatarajia kuanza kazi hiyo mara baada ya
kusaini mkataba baina ya Kampuni na Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Halmashauri hiyo ilivunja
Mkataba wa ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 8.6 kati yake na
Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam, baada ya Kampuni
hiyo kukiuka masharti ya mkataba wa miaka miwili uliomalizika Juni 30
mwaka 2017.
Baada ya muda huo kumalizika
Mkandarasi huyo aliingizwa kwenye tozo (Liquidated Damage) kwa siku 100 ambapo
Oktoba 8 mwaka jana ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zilimalizika hivyo
Manispaa ilivunja mkataba rasmi na Kampuni ya Lukolo.
Kadhalika baada ya kuvunjwa mkataba
huo, Manispaa ya Songea ilianza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi mwingine
ambapo amepatikana Mkandarasi wa Kampuni ya China Sichuan International ambaye
ataendeleza kazi ya ujenzi wa barabara na kwamba, Manispaa haijapata hasara
yeyote baada ya kuvunjwa kwa mkataba wa Mkandarasi wa kwanza.
Fedha za mradi huo ambazo ni zaidi ya
shilingi bilioni 14 zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea
uwezo Serikali za mitaa (ULGSP) ambapo mpango huo unakusudia kuendeleza
miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo ya
Songea.
Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi mwaka
2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka jana na kwamba barabara za Manispaa hiyo
ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2, barabara
ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya
Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Barabara nyingine ni Mitumbani hadi
Yapenda yenye urefu wa kilometa moja, barabara ya Polisi hadi Stendi ya
Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.
No comments:
Post a Comment