Mji wa Songea. |
Na Albano Midelo,
Songea.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) chini ya idara ya afya na ustawi wa jamii katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imeyafungia maduka ya dawa muhimu 48 kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya uendeshaji wa maduka hayo kisheria.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea, Dokta Mameritha Basike alisema kuwa idara ya afya imefanyakazi ya utambuzi wa maduka ya dawa muhimu ili kubaini iwapo maduka hayo, yanakidhi vigezo kulingana na mwongozo wa uendeshaji wa maduka ya dawa muhimu nchini.
Alisema kuwa kati ya maduka hayo yaliyofungiwa, maduka sita yamegundulika yanaendeshwa bila kibali na maduka 12 hayafanyi kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja licha ya kuwa na vibali vya kuendesha katika kuuza dawa muhimu.
Kwa mujibu wa Dokta Basike alieleza kuwa katika operesheni hiyo wamebaini maduka nane hayajahuisha vibali vya dawa muhimu kwa zaidi ya mwaka mmoja na maduka 22 yamefunguliwa katikati ya mji wa Songea kinyume cha muongozo ya maduka ya dawa muhimu.
Alisema kuwa imebainika kwamba maduka 23 bado hayajapata kibali cha Mfamasia isipokuwa yana barua iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ya kuruhusiwa kuendesha biashara ya duka la dawa muhimu.
“Kati ya maduka ya dawa muhimu 222 yaliyopo katika Halmashauri ya Manispaa hii ya Songea, ni maduka 146 ndiyo yana vibali vya kuendeshea biashara ya maduka ya dawa muhimu", alisema Dokta Basike.
Aliongeza kuwa katika operesheni ya utambuzi huo, maduka manne yamefungwa kwa sababu wamiliki wake wamefariki, wamiliki 11 wamepewa muda wa miezi sita maduka yao kupandishwa hadhi na kuwa maduka ya dawa moto (Famasi) kwa kuwa maduka yao yalifunguliwa mwaka 2003 kabla ya sheria ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ya mwaka 2003.
Manispaa hiyo imefanya utambuzi huo ili kutekeleza agizo la Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ya kuyatambua maduka ya dawa muhimu na rejareja yaliyosajiliwa chini ya Baraza la Famasia yanayoendeshwa kisheria.
Katika agizo hilo Katibu Mkuu ameagiza kuyaondoa kwa kuyafunga mara moja maduka yote ya dawa muhimu katika maeneo ya miji mikubwa yalioanzishwa kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment