Na Muhidin Amri,
Nyasa.
WAKALA wa majengo Tanzania (TBA)
kupitia kikosi chake cha ujenzi Mkoani Ruvuma, ameanza kazi ya ujenzi wa miradi
minne ya majengo ya Serikali Wilayani Nyasa Mkoani humo ambayo miradi hiyo
inagharimiwa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Meneja wa TBA Mkoani hapa, Mhandisi
Edwin Mnunduma alifafanua kuwa miradi yote minne inatekelezwa kwa kutumia
rasilimali zilizopo Serikalini kupitia wataalamu waliopo katika Ofisi ya Mkuu
wa mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya na Wakala wa majengo TBA.
Aidha alisema kuwa kikosi cha ujenzi huo
kinajenga majengo yake kwa kutumia njia ya kubuni na kujenga kwa pamoja ili kuweza
kutekeleza miradi ya Serikali kwa gharama nafuu.
Mnunduma alitaja miradi hiyo minne ni
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, nyumba ya makazi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri na Kituo cha afya kilichopo katika kata ya Kihagara.
Alibainisha kuwa mradi wa ujenzi wa
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambao ni wa ghorofa moja ulianza tangu mwezi Mei mwaka
jana na matarajio yake ni kukamilisha kazi hiyo mwezi Februari mwaka huu.
Kutokana na upatikanaji wa fedha kwa
awamu, mradi huo hivi sasa upo katika awamu ya kwanza ambapo gharama zilizotumika
ni shilingi milioni 199.9 na malipo husika yamekwisha fanyika.
Mhandisi huyo alibainisha kuwa mpaka
sasa malipo yaliyokwisha fanyika kwa Wakala ni shilingi milioni 80.7 sawa na
asilimia 50 ya mkataba na kazi zilizofanyika ikiwemo ujenzi wa nguzo, miamba
mlalo, kuezeka paa na uwekaji wa mabomba ya nyaya za umeme kwenye sakafu.
Alisema gharama za ujenzi wa Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa hadi kukamilika kwake yamefanyika makadirio kufikia kiasi
cha shilingi milioni 896.8 huku ujenzi wa ghorofa nyumba ya makazi nao
utagharimu shilingi 341.3, Ofisi ya Mkurugenzi shilingi bilioni 3.28 na Kituo cha
afya Kihagara ujenzi wake utakuwa ni wa shilingi milioni 585.5.
No comments:
Post a Comment