Na Muhidin Amri,
Madaba.
SERIKALI imetumia jumla ya shilingi milioni 500 kati ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma.
Kaimu Afisa mipango wa Halmashauri hiyo, Mwandishi Nchimbi alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu katika eneo ambalo ofisi hizo zinajengwa katika kitongoji cha Kifagulo kata ya Lituta Wilayani humo.
Nchimbi alisema kuwa jengo hilo linajengwa na Wakala wa majengo (TBA) mkoa wa Ruvuma na mara litakapokamilika litasaidia kwa kiasi kikubwa watumishi wa idara mbalimbali kuwa na ofisi zao kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za kila siku tofauti na ilivyokuwa hivi sasa ambapo wanalazimika kutumia jengo moja dogo la idara ya kilimo.
Kwa upande wake Meneja miradi wa TBA Mkoa wa Ruvuma ambaye ni msimamizi wa ujenzi huo, Ngulumi Magesa alisema kuwa tayari wamekwisha anza kuweka michoro ya jengo na kazi inayofuata sasa ni kuchimba mitaro kwa ajili ya kujenga msingi na nguzo.
Alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo utakuwa ni wa awamu mbili na utaendelea kutekelezwa kadri fedha zitakapopatikana kwani ni kati ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano mkoani Ruvuma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda mbali na kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi huo, ameitaka TBA wahakikishe kwamba wanafanya kazi usiku na mchana ili jengo hilo likamilike ujenzi wake kwa wakati na watumishi waweze kupata sehemu ya kufanyia kazi zao.
"Mimi kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Madaba naishukuru Serikali yetu ya awamu ya tano kwa uamuzi wake wa kutoa fedha za kujenga ofisi za halmashauri hapa kwetu, lakini nawaomba sana wenzetu hawa wa TBA wafanye kazi kama mchwa ili waweze kukamilisha kazi hii kwa wakati uliopangwa", alisema Mpenda.
No comments:
Post a Comment