Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI hapa nchini imetoa agizo kwamba, kwa wale wote viongozi ambao watabainika kwa namna moja au nyingine walishiriki kufanya ubadhirifu katika Chama Kikuu Cha Ushirika wa Kahawa (MBIFACU) kilichopo Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Aidha kufuatia agizo hilo askari kutoka Jeshi la Polisi Wilayani humo wamezingira Ofisi za MBIFACU zilizopo mjini hapa na kufunga makufuli ili ukaguzi wa mali za wanachama wa ushirika huo uweze kufanyika.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani hapa akihutubia wananchi wa Mbinga.
"Mimi mmenipatia jukumu la kuwatumikia hivyo ni lazima tuwatumikie, hatuhitaji kuona au kusikia mkulima wa kahawa hasongi mbele kimaendeleo", alisema Majaliwa.
Vilevile amewataka Madiwani wafanye kazi zao kwa weledi kwa kuwatumikia wananchi ipasavyo na kuacha migogoro isiyokuwa na tija kwa wananchi ambayo inarudisha nyuma maendeleo.
Majaliwa alisisitiza kuwa kilimo kikuukinachoweza kukuza uchumi wa wilaya ya Mbinga ni zao la kahawa, hivyo sasa maafisa ushirika waliopo katika wilaya hiyo wanapaswa kushirikiana pamoja kwa kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuzingatia misingi iliyowekwa na Serikali.
Kadhalika maafisa ushirika hao amewataka wahakikishe wanafanya sensa wilayani humo kwa lengo la kukusanya takwimu ambazo zitaweza kuifanya Serikali iweze kutambua wilaya inajumla ya wakulima wangapi ambao wanazalisha zao la kahawa.
Waziri Mkuu huyo alisisitiza kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu wahakikishe zoezi hilo limekamilika kwa wakati ili wakulima waweze kunufaika na kilimo hicho.
"Wajibu wa kusimamia maendeleo ya zao hili hivi sasa utafanywa na watumishi wa Serikali, Mkurugenzi mtendaji na Mkuu wa wilaya ninyi ndiyo wasimamizi na watendaji wakuu wa shughuli za Serikali naagiza ni lazima msimamie hili,
"Nendeni kwa wakulima vijijini ili tujue kila mkulima analoshamba lenye ukubwa gani tunabaki Serikali kulaumiana kwa sababu hatuna takwimu za wakulima wangapi wanaozalisha kahawa acheni kurundikana maofisini", alisisitiza.
Pia alibainisha anasikitishwa na taarifa zilizomfikia ofisini kwake kwamba, uzalishaji wa zao hilo Wilayani Mbinga umeanza kushuka kutokana na uzembe unaofanywa na maafisa kilimo na ushirika wa kutosimamia kikamilifu uzalishaji wa zao hilo.
No comments:
Post a Comment