Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANACHAMA wa kikundi cha Juhudi waliopo
katika kijiji cha Litumbandyosi kata ya Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga Mkoani
Ruvuma, ambao wanajishughulisha na kilimo cha zao la korosho wanatarajia
kuanzisha duka la pembejeo la zao hilo ili waweze kupata pembejeo kwa urahisi.
Mhasibu wa kikundi hicho, Athanas
Nyimbo aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa kuanzisha kwa duka hilo wanatarajia
kuanza na mtaji wa shilingi milioni mbili, fedha ambazo watapewa na Serikali
kutokana na mgawo wa asilimia 30 baada ya kazi waliyofanya ya uzalishaji wa
miche bora ya korosho ambayo itaanza kusambazwa kwa wakulima wa kijiji hicho.
Alisema kuwa kuanzishwa kwa duka hilo
itakuwa ni msaada mkubwa kwao katika kijiji hicho na maeneo mengine ya jirani
na kata ya Litumbandyosi, kwani hivi sasa wamekuwa wakilazimika kufuata huduma
ya pembejeo za korosho umbali mrefu Wilayani Tunduru.
Serikali imedhamiria kufufua na
kuendeleza zao la korosho pamoja na mazao mengine makubwa ya biashara ikiwemo
Pamba, tumbaku, chai na kahawa ambapo katika Wilaya ya Mbinga zao la korosho
limekuwa likistawi vizuri katika maeneo ya kata hiyo kutokana na kuwa na hali
ya hewa nzuri ya joto.
Nyimbo alieleza kuwa awali pembejeo
za zao hilo pamoja na kuzifuata mbali zimekuwa zikipatikana kidogo na
kwamba hazitoshelezi mahitaji halisi ya wakulima wake jambo ambalo limekuwa
likisababisha baadhi ya wakulima kukata tamaa kuendelea na kilimo cha zao la
korosho.
Aliongeza kuwa baada ya Serikali
kuhamasisha ufufuaji wa kilimo cha zao hilo hivi sasa idadi ya wakulima imezidi
kuongezeka kutoka 300 hadi kufikia wakulima 2,000 katika kijiji cha
Litumbandyosi na kwamba wanatarajia idadi hiyo kuzidi kuongeza hasa katika
msimu wa mwaka huu baada ya Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuanza
kuzalisha miche bora ya zao la korosho ambayo wakulima watagawiwa bure ili
waweze kuipanda katika mashamba yao.
Vilevile alisisitiza kuwa hivi sasa
wanaiomba Serikali kupitia wataalamu wake wa kilimo waliopo katika Halmashauri
za Wilaya, wapite vijijini mara kwa mara kwa wakulima kuwaelimisha juu ya mbinu
bora za kilimo cha zao hilo ikiwemo na matumizi sahihi ya pembejeo za zao la
korosho.
No comments:
Post a Comment