Wednesday, January 24, 2018

WANANCHI TUNDURU WAVAMIA SHAMBA LA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA



Na Mwandishi wetu,            
Tunduru.

BAADHI ya Wananchi kutoka vijiji mbalimbali Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, wamevamia shamba la Chama Kikuu cha Ushirika (TAMCU) kilichopo Wilayani humo kijiji cha Mtetesi, lenye ukubwa wa ekari 3,150 na kuanza kufanya shughuli mbalimbali za kilimo cha zao la korosho.

Mbali na kilimo hicho Waandishi wa habari wameshuhudia wavamizi hao maeneo mengine ya ardhi katika shamba hilo wakikata miti iliyohifadhiwa na Chama hicho huku wengine wakichoma mkaa jambo ambalo linatishia kutokea kwa uharibifu mkubwa wa mazingira.

Pia watu hao wameanza kupanda minazi, miembe, mahindi, mbaazi na matunda mbalimbali huku wakiendesha shughuli za ufugaji katika shamba hilo.

Kufuatia uvamizi huo, Wajumbe wa bodi ya TAMCU wamelazimika kutembelea shamba hilo na kuwakuta wananchi wakiwa wamegawana  maeneo na baadhi yao kuweka makazi ya kudumu  kwa kujenga nyumba za matofali na bati.


Akizungumza mara baada ya kujionea hali hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya mazao na mjumbe wa Bodi ya Wilayani Tunduru, Zainabu Yasini, amewataka wananchi kutofanya shughuli hizo za kudumu katika shamba hilo ili kuepuka hasara wanayoweza kuipata hapo baadaye ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao na kuharibiwa mali watakazokuwa wamewekeza.

Alisema jambo hilo la kusikitisha baadhi ya wananchi licha ya kutambua kuwa eneo hilo ni la Serikali, hata hivyo bado wameendelea kupuuza na kufanya shughuli hizo za kibinadamu ambapo amewataka waondoke ili kupisha uwekezaji mkubwa unaotarajiwa kufanyika katika shamba hilo katika msimu huu wa kilimo wa mwaka 2018/2019.

Aliongeza kuwa Chama hicho kinampango wa kufufua shamba hilo hasa baada ya Serikali kuweka mkakati wa kuboresha zao la korosho na kwamba kinakusudia kuliendeleza kwa kupanda miti mipya ya korosho ili katika kipindi cha miaka mitatu waweze kupata mapato ambayo yatasaidia kukiendesha chama kwa kulipa mishahara ya watumishi wake na mahitaji mengine.

Shamba la korosho la Mtetesi linalimikiwa na TAMCU Wilayani hapa tangu miaka ya 1980, lakini lilitelekezwa kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji wake hivyo kutoa nafasi kwa watu wengine kutoka maeneo mbalimbali kuvamia na kufanya shughuli zao.

No comments: