Na Mwandishi wetu,
Dar es Salaam.
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeviomba vyombo
vya kimataifa vinavyohusika na uangalizi wa haki za binadamu kuingilia kati
suala la uhuru wa kujieleza nchini.
LHRC pia imetaka Serikali kuheshimu Katiba kwa kutoingilia
uhuru wa kujieleza.
Kauli hiyo imetolewa leo siku moja baada ya Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuvitoza faini vituo vya televisheni vya ITV, Azam
Two, Startv, Channel Ten na EATV kwa kukiuka kanuni ya maudhui ya mwaka 2005.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dokta Hellen Kijo-Bisimba alisema
kuwa uamuzi wa kutozwa faini vituo hivyo ni ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya
habari wa kutoa taarifa kwa jamii na hasa zinazoikosoa Serikali.
"Serikali ikubali kuyasikiliza mazuri na mabaya na
kuyatumia maoni ya wananchi, vituo hivi vimetozwa faini kwa sababu vimetoa
taarifa ya tathmini iliyotolewa na LHRC kuhusu uchaguzi mdogo wa madiwani
uliofanyika Novemba mwaka jana”, alisema.
Dokta Kijo–Bisimba aliongeza kuwa, “Kwetu tunaona hili si
sawa na tunaona mambo haya yanazidi kuongezeka, Serikali kupitia Jeshi la
Polisi wamekuwa wakitumia neno uchochezi kuminya uhuru wa mawazo na kujieleza”.
Kutokana na hilo, LHRC ipo tayari kuungana na wadau ambao
wako tayari kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya neno uchochezi na baadhi ya
vifungu vya kanuni ya maudhui.
Dokta Kijo – Bisimba alieleza kuwa LHRC imeanzisha harambee
kuchangia gharama kuvisaidia vyombo vya habari vilivyokumbwa na adhabu hiyo.
No comments:
Post a Comment