Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Na Mwandishi wetu,
Tarime.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kusitisha uuzwaji wa mali za Chama
cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).
Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati
alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye
uwanja wa Serengeti Wilayani Tarime Mkoani hapa.
Hatua hiyo imekuja baada ya KNCU
kutangaza kuuza shamba lake kwa ajili ya kuiwezesha benki yake ya KCBL kutimiza
sharti la mtaji la Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Benki hiyo ya KCBL inatakiwa kutimiza
sharti la kuwa na mtaji kamili unaotosha wa shilingi bilioni 5 katika kipindi
cha miezi sita tangu kutolewa kwa tangazo hilo.
Waziri Mkuu, Majaliwa alisema kuwa ni
marufuku kuuza mali za ushirika huo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali
inafanya uhakiki wa mali za vyama mbalimbali vya ushirika hapa nchini.
Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria
kuimarisha ushirika nchini na sasa inafanya uhakiki wa mali za vyama vyote vya
ushirika na wale watakaobainika kuhusika na ubadhirifu watachukuliwa hatua.
Januari 4 mwaka huu BOT ilizipatia
miezi sita benki tatu hapa nchini ili ziweze kuongeza kiwango cha mtaji
unaohitajika, kutokana na matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji kamili wa
kutosha.
Benki hizo ni Kilimanjaro
Co-Operative Bank Limited, Tanzania Women Banki PLC na Tandahimba Community
Bank Limited na pale zitakaposhindwa kutekeleza agizo hilo zitachukuliwa hatua
ikiwemo kuzifutia leseni na kusimamisha shughuli za kibenki chini ya ufilisi,
iwapo benki hizo zitashindwa kutekeleza agizo hilo hadi kufikia Juni 30, 2018.
No comments:
Post a Comment