Msafara wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ulipowasili Januari 5 mwaka huu katika eneo la Kituo cha utafiti wa zao la kahawa (TaCRI) Ugano Wilayani Mbinga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa Serikali itaona namna bora ya kusaidia Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa (TaCRI) katika kituo chake cha Ugano kilichopo Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, ili taasisi hiyo iweze kuzalisha miche kwa wingi na kuisambaza kwa wakulima wake.
Aidha licha ya Serikali kuzipatia halmashauri fedha nyingi hasa kwa sekta ya kilimo, lakini wameshindwa kuzalisha miche kama TACRI inavyofanya huku Watendaji wa idara ya kilimo wametakiwa kubadilika kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema hayo Januari 5 mwaka huu wakati alipokuwa kwenye ziara yake Wilayani hapa na alipotembelea kituo hicho cha utafiti wa zao la kahawa.
Majaliwa alisema kuwa umefika wakati sasa kwa wataalamu wa kilimo hapa nchini katika maeneo mbalimbali, wanapaswa kubadilika na sio muda mwingi wakionekana kukaa maofisini na kupika taarifa kwamba, wamewahudumia wakulima vijijini badala yake wanapaswa kwenda huko na kuishi karibu na wananchi.
Akiwa katika kituo hicho cha utafiti wa zao la kahawa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa TaCRI nchini, Deusdedit Kilambo alimweleza Waziri Mkuu, Majaliwa kuwa taasisi hiyo imeendelea na mkakati wake wa kuainisha teknolojia zitakazochangia kuongeza tija na ubora wa zao hilo.
Kilambo alifafanua kuwa katika kufanya hayo imesaidia kupunguza gharama za uzalishaji ili kuboresha kipato na riziki kwa mkulima ambapo kahawa miche aina ya vikonyo, imekuwa ikizalishwa ambayo haishambuliwi na wadudu kwa urahisi ambapo vikundi vya wakulima vimekuwa vikifundishwa pia namna bora ya uzalishaji wa miche hiyo jambo ambalo limepata mafanikio makubwa.
Alibainisha kuwa taasisi imekuwa ikiendelea kutafiti pia aina za kahawa zenye tija kubwa zaidi, ukinzani kwa magonjwa na ubora unaokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi ikiwemo uzalishaji miche kwa njia ya chupa (Tissue culture).
"Ushauri juu ya kuboresha rutuba ya udongo pamoja na matumizi ya mbinu shirikishi za kudhibiti wadudu waharibifu wa kahawa ili kuongeza tija na kipato umefanywa katika maeneo husika", alisema Kilambo.
Vilevile jumla ya wakulima 377,496 na maafisa ugani 10,865 wamepata mafunzo kuhusu kanuni bora za kilimo cha kahawa na uzalishaji wa miche hiyo.
Kadhalika bustani 400 zimeanzishwa nchi nzima kati ya hizo bustani 95 zipo kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe na Iringa ambapo wataalamu waliopo katika maeneo hayo hushirikiana na TaCRI katika kuzalisha miche chotara ya kahawa.
Hata hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali licha ya uwepo wa ufinyu wa bajeti, jumla ya miche 15,885,051 ya aina bora chotara ya kahawa imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika mikoa hiyo.
No comments:
Post a Comment