Na Mwandishi wetu,
UWEPO wa madai ya harufu ya ufisadi
ambao unadaiwa kufanyika katika kitengo cha Manunuzi katika Chuo Kikuu cha
Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) kumefanya Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kuagiza ufanyike uchunguzi ili kuweza
kuwabaini wahusika na hatimaye wachukuliwe hatua za kisheria.
Profesa Joyce Ndalichako. |
Wakati hilo likiendelea kutekelezwa
pia Waziri huyo ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mkuu anayehusika na kitengo hicho,
pamoja na kuchunguzwa kwa wale wote wengine watakaohusika katika sakata hilo.
Hatua hiyo iliyochukuliwa na Profesa
Ndalichako ilitokea juzi alipofanya ziara yake ya kushtukiza katika taasisi
hiyo, kwa lengo la kujionea na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo.
Kadhalika uwepo wa ziara hiyo
ulitokana na kubaini pia matumizi mabaya ya fedha za umma, ndipo ilimlazimu
Waziri kufanya hivyo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua na kukomesha hali
hiyo isiweze kujirudia tena.
Profesa Ndalichako alifafanua kuwa
awali aliunda Kamati ndogo iliyokuwa inafuatilia tuhuma hizo na baadaye majibu
aliyoyapata yalionesha kuna harufu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika
kitengo hicho cha manunuzi.
“Tunapofika kwenye suala la manunuzi
kwenye taasisi hii hakuna ushindani, badala yake kazi anapewa mtu mmoja kupitia
kampuni tatu tofauti, nimefanya uchunguzi wangu nimebaini kuna kampuni tatu
ambazo zote zinamilikiwa na mtu mmoja ndizo zinazopata zabuni ya ununuzi katika
chuo hiki, hakuna mchakato wa kushindanisha kampuni kama zinavyoagiza sheria za
manunuzi Serikalini”, alisema.
Vilevile pamoja na kuagiza Wakuu wa
idara kuwa makini katika uagizaji wa vitu kulingana na mahitaji, Profesa
Ndalichako alisema mbele ya uongozi wa MUHAS huku akimwagiza Mwenyekiti wa bodi
ya chuo hicho, Mariam Mwaffisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kuwanasa
wale wote waliohusika na vitendo hivyo.
“Ninaagiza kusimamishwa kazi kwa Mkuu
huyu wa kitengo lakini si ajabu wapo wengine mapapa, Mwenyekiti nitakukabidhi
makabrasha yote niliyoyapata kutokana na uchunguzi wangu, fuatilieni hata kama
ni Makamu Mkuu wa chuo, kama amehusika awajibishwe msimuogope mtu”,
alisisitiza.
No comments:
Post a Comment