Friday, January 19, 2018

BREAKING NEWS: WAZAZI KIPIKA WAKUSANYIKA NA KUDAI WAPEWE FEDHA ZAO WALIZOCHANGISHWA KWA AJILI YA CHAKULA CHA WATOTO SHULENI


Baadhi ya Wazazi wakiwa wamekusanyika leo katika eneo la shule ya msingi Kipika Halmashauri Mji wa Mbinga wakishinikiza kupewa fedha zao, walizochangishwa kwa ajili ya chakula kwa watoto wao wanaosoma shuleni hapo.


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KUFUATIA tamko la Rais Dokta John Pombe Magufuli la kusitisha michango kwa shule za Msingi na Sekondari hapa nchini, baadhi ya Wakazi wanaoishi katika mtaa wa Matarawe Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma wamekusanyika katika eneo la viwanja vya shule ya msingi Kipika, iliyopo mjini hapa na kudai warudishiwe michango yao ya fedha walizochangishwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu.

Tukio hilo limetokea leo Januari 19 mwaka huu majira ya asubuhi ambapo wakazi hao ambao ni wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni hapo, walikusanyika katika eneo hilo baada ya Diwani wao wa kata hiyo Leonard Mshunju kuitisha mkutano wa dharula ili kuweza kujua hatma ya michango ya fedha, mahindi na maharagwe ambayo walichangishwa kwa ajili ya chakula cha watoto wanaosoma shuleni hapo.

Mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo, wakichangia hoja kwa nyakati tofauti wazazi hao walisema kuwa wao hawawezi kupingana na tamko lililotolewa na Rais Dokta Magufuli kwani wakati wanachangishwa michango hiyo baadhi yao walikuwa wakipewa vitisho huku wengine watoto wao wakikosa nafasi ya kuandikishwa kuanza shule darasa la awali kutokana na kukosa mchango husika.


“Wakati mlipotushirikisha katika zoezi hili la kuchangisha fedha na chakula kwa watoto wetu tulikubaliana, lakini wengine mlikuwa mkitupatia vitisho na maneno yasiyokuwa na busara kumbe leo hii elimu inatolewa bure na bado mnataka tutoe michango kwa lazima maana yake nini, tunataka turudishiwe michango yetu”, walisema. 

Akizungumza kwa lengo la kutetea hoja zilizotolewa na wazazi hao katika mkutano huo, Mwenyekiti wa shule hiyo Job Mbelle alisema kuwa hakuna mtoto aliyefukuzwa au kutoandikishwa kwa ajili ya kuanza masomo shuleni hapo kutokana na mzazi kukosa mchango.

Baada ya Mwenyekiti huyo kuzungumza hayo, bado wazazi hao walionekana kuja juu huku wakizomea na kusema sio kweli kwani baadhi yao wamefanyiwa vitendo hivyo.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Matarawe, Mshunju aliwataka wazazi hao watulie na baadaye alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kutaka kufikia muafaka juu ya michango yao waliyochangishwa ya chakula na fedha warudishiwe au la.

“Ndugu wazazi wote tumesikia kwenye vyombo vya habari kwamba michango yote imezuiwa, kwa wale wote ambao walichangia wanatakiwa warudishiwe michango yao pia Mheshimiwa Rais amesema kwa mzazi ambaye atajisikia kuchangia kuanzia sasa, apeleke mchango wake mwenyewe kwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kwa hiari na sio lazima,

“Hakuna mtu yeyote kumlazimisha kuchangia chochote kile, kila mtu awe huru afanye kitu kwa hiari yake”,  alisema Mshunju.

Pamoja na mambo mengine, baada ya mvutano wa muda mrefu wazazi hao walifikia muafaka kwamba watarejeshewa michango yao waliyochangia ifikapo siku ya Jumatatu Januari 22 mwaka huu wakaichukue shuleni hapo.

Kufuatia hali hiyo, Mwandishi wetu alibaini kuwa pamoja na wazazi hao kuchangishwa michango hiyo katika shule hiyo ya msingi Kipika hapakuwa na risiti yoyote iliyokuwa ikitolewa na kwamba michango hiyo ilianza kukusanywa Novemba 30 mwaka jana na mwisho ilikuwa ni Januari 8 mwaka huu.

Hata hivyo ukusanyaji wa michango hiyo ulikuwa ukifanyika kwa mwaka mzima wazazi wenye watoto kuanzia darasa la awali walikuwa wakichangia shilingi 10,000 darasa la kwanza, la pili mpaka la saba shilingi 5,000 pamoja na dumla mbili za mahindi na maharagwe.

No comments: