Na Kassian Nyandindi,
Tunduru.
SERIKALI Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma,
imeiomba Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuangalia uwezekano wa kuipatia Wilaya
hiyo fedha shilingi milioni 300 ambazo iliomba, kwa ajili ya kusaidia
kuharakisha utekelezaji wa ujenzi miundombinu ya maji katika mji wa Tunduru.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Homera
alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake
juu ya maendeleo mbalimbali ya ujenzi wa miradi ya maji katika mji huo.
Homera alifafanua kuwa maombi hayo
yalitokana na Mamlaka ya maji mjini hapa kuelemewa na ubovu wa miundombinu yake
hali ambayo husababisha wananchi kutumia maji yasiyokuwa safi na salama.
Alisema kuwa fedha hizo ni maombi ya
mwaka wa bajeti wa 2017/2018 kwa Wizara
hiyo, kwa ajili ya kuweza kusaidia kuboresha miundombinu hiyo ili kuweza kufikia
lengo la asilimia 90 ya upatikanaji wa maji hayo.
Vilevile Mkuu huyo wa Wilaya aliishukuru
Wizara kwa kuipatia Wilaya ya Tunduru kwa kuipatia fedha shilingi milioni 300
katika bajeti yake ya mwaka 2016/2017 ambayo imewezesha kuongeza na kuboresha upatikanaji
wa huduma ya maji kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 60.
Alisema kuwa fedha hizo zilitumika
kuimarisha miundombinu ya maji katika mji huo kwa kusambaza mtandao mpya wa
mabomba ya maji wenye urefu wa kilometa tisa na kufanya mtandao huo kufikia kilometa
34 tofauti na awali ambapo ulikuwa na urefu wa kilometa 25.
“Tukipata fedha hizo zitasaidia kwa kiasi
kikubwa kumaliza tatizo la maji katika mji wetu wa Tunduru, bado tunayoshida
katika sekta hii ya maji na Serikali sasa inaendelea kuhakikisha inamaliza
changamoto zilizopo ili wananchi watumie muda wao kwa ajili ya kufanya kazi za kukuza
uchumi badala ya kuhangaika muda mwingi kutafuta maji mbali na makazi yao”, alisema
Homera.
Pia akizungumzia utekeleza wa miradi
ya maji katika vijiji mbalimbali vilivyopo wilayani humo, alieleza kuwa
Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo imeweza kuchimba
visima virefu 35 ikiwa ni juhudi za Mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha kwamba anasogeza
huduma bora ya maji karibu na wananchi.
Katika utekelezaji huo Halmashauri ya
wilaya hiyo kupitia mapato yake ya ndani, fedha kutoka Serikali kuu katika
kipindi cha miaka miwili imetumia zaidi ya shilingi milioni 112 kwa ajili ya
kufanikisha uboreshaji wa miundombinu ya maji, kwenye vijiji na Kata mbalimbali
Wilayani humo.
Alisema kuwa fedha hizo zilitumika
kuchimba visima virefu, kukarabati na kufunga mashine za kusukuma maji katika
shule za Sekondari, zahanati pamoja na vituo vya afya kwa ajili ya kusaidia
uboreshaji wa huduma husika.
Kadhalika katika utekelezaji huo
wadau wa maendeleo kupitia shirika la AMCC kutoka nchini Canada wamechimba
visima 25 katika vijiji 67 vilivyopo katika kata 16 Wilayani Tunduru na
kusaidia kupunguza tatizo la maji kutoka asilimia 40 hadi 75.
Hata hivyo aliongeza kuwa kabla ya
utekelezaji wa miradi hiyo wananchi wengi walikuwa wakichota maji katika mito
na visima vifupi wakinyang’anyana na wanyama wakali kama vile simba, tembo,
chui, nyoka na fisi.
No comments:
Post a Comment