Monday, January 8, 2018

SERIKALI YATUPILIA MBALI PENDEKEZO LA MADIWANI MBINGA UJENZI WA OFISI NDENGU

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

SERIKALI hapa nchini imefuta mapendekezo ya ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, katika eneo la Ndengu lililopo kata ya Nyoni Wilayani humo ambayo yalipitishwa hivi karibuni na Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.

Mapendekezo hayo yalifutwa juzi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi na Madiwani wa halmashauri ya Wilaya hiyo katika ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Waziri Mkuu, Majaliwa alisema kuwa eneo hilo ambalo wanataka kujenga ofisi hizo, limetengwa na kuhifadhiwa kwa miaka mingi kwa ajili ya kutunza mazingira na vyanzo vya maji vilivyopo huko ambavyo ndiyo tegemeo kubwa kwa ajili ya kulisha wakazi wa mji wa Mbinga.


Alisema mgogoro uliopo sasa wa Madiwani kugombana wapi wakajenge ofisi hizo unapaswa kwisha na Serikali ilikwisha waletea fedha siku nyingi za kujenga majengo ya ofisi hizo lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.

"Halmashauri ya Wilaya mnao mgogoro wa kugombania eneo lililotengwa kwa ajili ya vyanzo vya maji ni wapi mkajenge ofisi zenu, hivyo kuanzia sasa ni marufuku kwenda kujenga ofisi pale tafuteni kiwanja jengeni ofisi hapa hapa mjini", alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Vilevile alimtaka Afisa misitu wa halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwenda katika eneo la msitu wa Ndengu na kuendelea na shughuli ya upandaji wa miti ili kuweza kuimarisha uoto wa asili katika hifadhi hiyo ya vyanzo vya maji.

Kwa ujumla halmashauri ya Wilaya hiyo imefikia hatua ya kuhama katika ofisi zake za awali zilizopo mjini hapa na kwenda kujenga miundombinu mingine mipya ya Wilaya hiyo katika eneo jingine, baada ya kugawika na kuizaa halmashauri nyingine ya Mji wa Mbinga ambayo ndiyo inapaswa kutumia majengo hayo yaliyopo sasa mjini hapa.

No comments: