Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
NAIBU Waziri wa ujenzi, Elias
Kwandikwa amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la mto Ruhuhu Wilayani Nyasa Mkoa
wa Ruvuma kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba anamaliza ujenzi
wa daraja hilo kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Kwandikwa alitoa agizo hilo alipokuwa
Wilayani humo akikagua ujenzi wa daraja hilo ambapo ameusisitiza Uongozi wa
Wakala wa Barabara (TANROADS) Makao makuu, kuhakikisha kwamba utaratibu wa
zoezi zima la ununuzi wa vyuma vitakavyowekwa juu ya daraja hilo unaenda
sambamba na makadirio ya muda wa mradi ili kufanya kazi hiyo ikamilike kwa muda
uliopangwa.
“Nafikiri sasa jipangeni vizuri ili
masika yanapokwisha mhakikishe mnafanya kazi kwa bidii ya hali ya juu, nataka
kufikia mwezi Juni mwaka huu daraja liwe limekamilika, pia TANROADS Makao makuu
hakikisheni mchakato wa manunuzi ya vyuma vya daraja hili mnauanza mapema ili
kuweza kukamilisha mapema”, alisisitiza.
Vilevile alieleza kuwa daraja hilo ujenzi
wake utakapokuwa umekamilika utakuwa ni kiungo muhimu kwa watu wa Nyasa Mkoani
Ruvuma na Ludewa Mkoa wa Njombe, kwani wamekuwa wakilisubiri daraja hilo kwa
ajili ya kujiendeleza katika shughuli zao mbalimbali za kukuza uchumi.
Pia amemwagiza Meneja wa Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoani Ruvuma, Mhandisi Elisha Mgira, kuhakikisha kwamba
anarekebisha kasoro zilizopo kwenye kivuko cha mto Ruhuhu ili kuweza kufanya
kazi hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wanasubiri ujenzi wa daraja hili
ukamilike.
Kwa upande wake Mhandisi Mkazi wa
daraja hilo, Mhandisi Napegwa Kiseko naye alisema kuwa ujenzi wa mradi huo
umefikia asilimia 50 ambapo kazi zinazofanyika hivi sasa ni kujaza matabaka ya
barabara zinazoingia darajani hapo ili kunyanyua tuta la barabara.
Napegwa alifafanua kuwa kazi hiyo
inaendelea pande zote mbili yaani mkoa wa Ruvuma na Njombe, ingawa kwa kipindi
hiki cha mvua kazi hiyo imekuwa na vikwazo vingi.
Alisema kuwa ujenzi wa misingi ya
daraja kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma upo kwenye hatua za mwisho na Njombe ujenzi
ulianza mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana na bado unaendelea.
Mradi wa ujenzi wa daraja la mto
Ruhuhu ambao upo mpakani mwa Mkoa wa Ruvuma na Njombe unatarajiwa kugharimu kiasi
cha shilingi Bilioni 6 ambazo ni fedha za Serikali kwa asilimia mia moja na
unatarajiwa kukamilka mwezi Juni mwaka huu.
No comments:
Post a Comment