Na Muhidin Amri,
Madaba.
WANANCHI wa vijiji viwili vya Magingo na Mkongotema Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na Serikali wamefanikiwa kujenga zahanati ili waweze kupata huduma bora za matibabu karibu na makazi yao.
Aidha imeelezwa kwamba ujenzi wa zahanati hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa huduma za watoto na akina mama wajawazito kuweza kujifungua sehemu salama na kupata huduma nyingine za uzazi katika mazingira salama badala ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Magingo, Kwinbert Mhoro alisema hayo juzi alipokuwa akizungumzia kuhusiana na ujenzi wa zahanati hiyo mbele ya waandishi wa habari.
Alisema kuwa hadi sasa wamefanikiwa kukamilisha vyumba naneb kati ya 14 vinavyohitajika na kwamba kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kumaliza kero ya muda mrefu ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya kwenda vijiji vya Lutukira au Madaba.
Mhoro alisema kutokana na Mpango wa Afya ya Msingi (MMAM)ambao unataka kila kata kuwa na kituo cha afya, wamekusudia hapo baadaye zahanati hiyo kubadili na kuwa kituo cha afya.
Alibainisha kuwa tayari wamekwishaketi vikao mbalimbali kwa ajili ya kupitisha maamuzi hayo na wamefikia hatua nzuri kwa sababu hata huduma zitakazotolewa zitakuwa bora zaidi ikilinganishwa na zile zitakazotolewa kwenye zahanati.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake, mmoja wa akina mama wa kijiji cha Magingo Debora Mgaya ameiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma, itoe fedha ili kuweza kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo ambayo ikikamilika itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Madaba.
No comments:
Post a Comment