Rais Dokta John Pombe Magufuli. |
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Jaji Mkuu wa
Tanzania, Ibrahim Juma kutokana na kifo cha Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani,
Robert Kisanga.
Jaji Kisanga alifariki dunia jana Jumanne
Januari 23 mwaka huu katika Hospitali ya Regency Jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa leo Januari
24 mwaka huu imemnukuu Dokta Magufuli akisema kuwa Jaji Kisanga atakumbukwa kwa
mchango wake alioutoa kwa Taifa hili wakati wote wa utumishi wake.
Dokta Magufuli alisema kuwa utumishi
wa Jaji Kisanga ulijaa umakini, uchapakazi, uzalendo na ushirikiano kwa
wengine, mambo ambayo yalimwezesha kupata mafanikio makubwa.
“Sote tunafahamu kazi nzuri
alizofanya akiwa katika majukumu ya kitaifa, mchango wake katika kuijenga
taaluma ya uanasheria baada ya uhuru na uanzishaji wa Mahakama ya Rufani baada
ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, kwa hakika mchango wake
hautasahaulika”, alisema.
Kadhalika alimuomba Profesa Juma
kufikisha rambirambi hizo kwa familia ya Jaji Kisanga, majaji na wanasheria
wote, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo.
Hata hivyo amewaomba wafiwa kuwa na
moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
No comments:
Post a Comment