Dokta John Pombe Magufuli. |
Na Mwandishi wetu,
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ametoa agizo la kusitishwa kwa usajili wa
meli mpya hapa nchini, kufuatia taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya na
bidhaa nyingine zinazopingwa kimataifa katika meli hizo ambazo zinapeperusha
bendera ya Tanzania na sasa zimefikia tano.
Dokta Magufuli ametoa agizo hilo jana
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume.
Kadhalika amemtaka Waziri wa mambo ya
nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga kusimamia
utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha jina la Tanzania halichafuliwi ndani
na nje ya nchi.
Pia taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano
Ikulu imeeleza kuwa agizo hilo lilitolewa wakati Rais akifanya mazungumzo na
wafanyakazi wa Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye
ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) ambapo mawaziri hao
nao walikuwepo.
“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli
zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli
zilizokamatwa ambazo ni tano na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinaendelea
kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na
watu wanaofanya mambo kwa maslahi yao”, alisema Dokta Magufuli.
Vilevile alihimiza kutekelezwa kwa
maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu, ambaye alitangaza
kuzifutia usajili wa meli mbili zilizokamatwa sanjari na kuamuliwa kushusha
bendera ya Tanzania.
Suluhu alizitajia meli hizo kuwa ni
Kaluba yenye usajili wa namba IMO6828753 iliyokamatwa maeneo ya Jamhuri ya
Dominican Desemba 27 mwaka jana, ikiwa na wastani wa tani 1.6 ya dawa za
kulevya pamoja na Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa
ikisafirisha silaha kinyume na sheria za kimataifa.
No comments:
Post a Comment